Diwani mteule wa Chama cha ACT Wazalendo, Juma Mzee Shaban, amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Kigoma pamoja na wenzake kumi, wakikabiliwa na kesi ya ujambazi wa kutumia silaha, kinyume na kifungu cha 287 cha Kanuni ya Adhabu (Sura ya 16, Marejeo ya 2023).
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, imeelezwa kuwa mnamo tarehe 30 Oktoba 2025, katika eneo la Kagera, ndani ya Wilaya na Mkoa wa Kigoma, washtakiwa hao, wakiwa pamoja na wengine ambao bado hawajakamatwa, walitenda kosa la kuwasha moto na kuchoma Ofisi ya Mtendaji wa Kata ya Kagera yenye thamani ya shilingi 59,323,800, mali ya Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma.
Taarifa zinaeleza kuwa wanachama 117 wa ACT Wazalendo walikamatwa siku ya uchaguzi na siku ya maandamano, akiwemo mgombea ubunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe. Baada ya mahojiano, wanachama 102 waliachiwa huru akiwemo Zitto Kabwe, huku 15 wakibaki rumande.
Miongoni mwa waliobaki, 11 wamefunguliwa kesi hiyo ya ujambazi, na wanne wameendelea kushikiliwa kwa uchunguzi zaidi. Inadaiwa pia kuwa wanachama na viongozi wengine wa chama hicho wamekimbia na hawajulikani walipo, wakihofia kukamatwa.
Kesi hiyo, yenye namba ya jinai 26490 ya mwaka 2025, inaendelea kusikilizwa katika Mahakama ya Wilaya ya Kigoma.






0 Comments