Matukio Daima, Morogoro
WANAFUNZI wawili wameingia matatani Mjini Morogoro kwa kuhusishwa na Matukio mawili tofauti yaliyozua simanzi na taharuki, mmoja akiuawa na mwingine akijaribu kujiua.
Matukio haya yaliyothibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro SACP Alex Mkama yamewahusisha wanafunzi wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Mgulasi, Valerian Nicholas (18), aliyefariki dunia baada ya kushambuliwa na wananchi akidaiwa kujaribu kuiba simu, huku mwanafunzi mwingine wa Chuo Kikuu cha Waislamu Morogoro (MUM), Goodluck Charles Jactad (26), akinusurika kifo baada ya kujaribu kujiua.
Tukio la Valerian lilitokea maeneo ya Chakabovu kata ya Chamwino manispaa ya Morogoro wakati akidaiwa kuwa kwenye jaribio la uporaji wa simu kwa kutumia pikipiki maarufu kama kishandu.
Wananchi wenye hasira walimvamia na kumshambulia, na baadaye alifariki dunia kutokana na majeraha hayo.
Kijana huyo alipaswa kuungana na wenzake walioanza mitihani ya kidato cha nne siku ya jumatatu, ambapo mwenzake alikimbia na Bado anatafutwa na Polisi.
Jeshi la Polisi kupitia Kamanda wa Polisi wa Mkoa SACP Alex Mkama, limekemea vikali kitendo cha wananchi kujichukulia sheria mkononi huku wakionya vijana kutafuta shughuli halali za kujiingizia kipato badala ya kujiingiza kwenye Matukio yanayotishia usalama wao.
Katika tukio jingine, mwanafunzi wa chuo kikuu cha Waislam Morogoro MUM, Goodluck Charles Jactad, amejijeruhi vibaya usiku wa Novemba 16 baada ya kujikata shingoni kwa kitu chenye makali akiwa maeneo ya Msamvu.
Alikimbizwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro na anaendelea kupatiwa matibabu akiwa chini ya ulinzi wa Polisi huku chanzo cha tukio kikichunguzwa.
Wakati hayo yakitokea, Polisi imebainisha tukio jingine lililohusisha kukamatwa kwa Shiwa Juma Malisha (29), mkazi wa Biro – Malinyi, kwa tuhuma za kumuua Masanja Manzegeya Zengo (46) katika eneo la Mlole, Misesege, usiku wa Novemba 15.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro amewataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano na kujiepusha na vitendo vya kujichukulia sheria, akisisitiza kuwa oparesheni dhidi ya uhalifu zinaendelea kwa nguvu zote.





0 Comments