Na Matukio Daima Media
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, amesema yuko tayari kuitwa na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ili kujibu tuhuma zinazomhusisha na umiliki wa vituo vya mafuta vya Lake Oil.
Amesema hayo alipokuwa akizungumza na watumishi wa wizara hiyo Novemba 26, 2025, akibainisha kuwa ni muhimu taarifa za watumishi wa umma kuwa wazi.
Amesisitiza kuwa pale panapojitokeza sintofahamu, viongozi wanapaswa kuhojiwa na taarifa kuwekwa hadharani ili wananchi wapate ukweli.
“Malalamiko juu ya viongozi yamekuwa mengi sana; haijulikani lipi ni kweli na lipi si kweli,” amesema.
Akitoa mfano, Ridhiwani amesema maandamano yaliyotokea hivi karibuni yalihusisha malalamiko kuhusu maadili ya viongozi, ambapo ilidaiwa kuwa vituo vya mafuta vinavyojulikana kama Lake Oil vinamilikiwa naye.
“Kuna mtu mmoja anaitwa Ali Edha; ana vituo vya mafuta vinavyoitwa Lake Oil, lakini vimechomwa kwa madai kuwa ni vya Ridhiwani,” amesema.
Ridhiwani aliitaka tume hiyo kumuita bila hofu ili kumhoji, huku akipendekeza uchunguzi ufanyike kwanza na baada ya kukamilika waandaliwe waandishi wa habari.
Pia ameshauri tume iombe ushahidi wa ziada kutoka kwa umma ili kuweka ukweli hadharani.





0 Comments