Na Matukio Daima Media Iringa
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Kheri James, amesema kuwa hali ya usalama katika mkoa huo imeendelea kuwa shwari katika wilaya zote, zikiwemo Iringa, Mufindi na Kilolo, huku shughuli za kijamii na kiuchumi zikiendelea kama kawaida. Amesema kuwa wananchi wameendelea kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha amani na utulivu vinaendelea kudumishwa katika maeneo yote ya mkoa huo.
Akizungumza leo 6 Novemba, 2025 wakati wa ziara yake katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Lugalo iliyopo wilayani Kilolo, Mkuu huyo wa Mkoa alisema kuwa amejiridhisha kuona kuwa hali ya maisha ya wananchi imerejea katika utaratibu wa kawaida na hakuna viashiria vyovyote vinavyoweza kutishia amani.
Kheri James alibainisha kuwa katika kipindi cha hivi karibuni, serikali kwa kushirikiana na vyombo vya dola imechukua hatua madhubuti za kuhakikisha usalama wa wananchi na mali zao, hali iliyochangia kurudi kwa shughuli mbalimbali za maendeleo. “Leo nimefanya ziara katika wilaya zote tatu za Iringa, Mufindi na Kilolo, na ninapenda kuthibitisha kuwa hali ya usalama ni tulivu, wananchi wanaendelea na shughuli zao za kila siku bila hofu yoyote,” alisema.
Aidha, aliongeza kuwa huduma zote za msingi kama vile afya, elimu, maji na miundombinu ya barabara zinaendelea kutolewa ipasavyo, na serikali ya mkoa inaendelea kuhakikisha kuwa taasisi zote za umma zinafanya kazi kwa ufanisi. Alitoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na serikali katika kulinda amani, akisisitiza kuwa maendeleo hayawezi kupatikana bila kuwepo kwa utulivu na mshikamano katika jamii.
Mkuu huyo wa Mkoa pia alipongeza juhudi za walimu na wanafunzi kwa kuendelea na masomo kwa bidii licha ya changamoto ndogo ndogo zilizojitokeza katika baadhi ya maeneo, akisema kuwa shule zote za msingi na sekondari zimeendelea na ratiba zao za kawaida bila usumbufu wowote. “Nimefurahishwa kuona wanafunzi wakiendelea na masomo, na walimu wakiwa katika nafasi zao wakitekeleza majukumu yao hii ni dalili ya uthabiti wa jamii yetu,” alisisitiza.
Katika ziara hiyo, Mhe. Kheri James aliambatana na viongozi wa usalama wa mkoa, maafisa elimu na viongozi wa serikali za mitaa, ambapo walipokea taarifa za maendeleo kutoka kwa wakuu wa wilaya na wakurugenzi watendaji wa halmashauri.
Kwa upande wao, wananchi wa maeneo alikotembelea walimpongeza Mkuu wa Mkoa kwa kufuatilia kwa karibu hali ya usalama na maendeleo ya jamii, wakisema kuwa hatua hiyo imewapa matumaini na kuimarisha imani yao kwa serikali.
Mkoa wa Iringa umekuwa miongoni mwa mikoa inayoongoza kwa kuwa na utulivu na mshikamano mkubwa wa kijamii, jambo ambalo limechangia kuvutia wawekezaji na kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi katika sekta mbalimbali kama kilimo, elimu, utalii na biashara.
Ziara ya Mkuu wa Mkoa imeonesha kuwa Iringa inaendelea kuwa mfano wa mkoa salama na wenye dira ya maendeleo endelevu, chini ya usimamizi makini wa serikali na ushirikiano wa wananchi wake.






0 Comments