Header Ads Widget

NAIBU WAZIRI WANU AFANYA ZIARA DIT

Na Mwandishi Wetu.

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Wanu Hafidhu Amir, amepongeza uongozi wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) kwa usimamizi mzuri na uendeshaji wa Chuo cha Ufundi Dodoma (DTC).

Mhe. Naibu Waziri ametoa pongezi hizo alipotembelea DIT Kampasi ya Dodoma leo, ambapo ameeleza kuridhishwa kwake na ubora wa miundombinu ya kampasi hiyo, akibainisha kuwa mazingira hayo yanaashiria kuwa DIT itazalisha wataalam wenye ujuzi katika masuala ya teknolojia ya anga.

“Nimeridhishwa na ubora wa majengo kuanzia kwenye ujenzi na hata ukubwa wake kwa kweli unaridhisha. Kwa hiyo sasa naamini hapa tutapata wataalam wenye ujuzi mkubwa kwenye mambo ya anga, yaani ‘Space and Allied Technology’,” amesema Mhe. Naibu Waziri.

Katika hotuba yake, Wanu amesisitiza kwamba lengo kuu la Serikali ni kuhakikisha Tanzania inakuwa taifa lenye vijana wanaoajirika katika masoko ya ndani na kimataifa kupitia ujuzi, umahiri na matumizi ya teknolojia zinazochochea ubunifu na ushindani.

Ameongeza kuwa DIT inaendelea kutoa fursa muhimu kwa vijana kupata stadi za kazi zitakazowawezesha kujiajiri.

Aidha, Mhe. Wanu amepongeza jitihada za DIT katika kuanza kushiriki kwenye miradi ya utafiti wa uundaji na urushaji wa satelaiti ya kwanza ya Tanzania, akibainisha kuwa hatua hiyo inaendana na mipango ya Serikali ya kujenga uwezo katika teknolojia ya anga kwa lengo la kutatua changamoto za kijamii.

Kwa upande wake, Mkuu wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Prof. Preksedis Marco Ndomba, ameishukuru Wizara kwa kuiamini DIT na kukikabidhi chuo hicho jukumu muhimu la usimamizi. Amesema Kampasi ya Dodoma itaendelea kujikita katika kutoa programu maalum za anga, na kwamba matarajio ni kuona DTC ikiendeleza jitihada hizo kwa ufanisi mkubwa.







Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI