Header Ads Widget

SONGWE KUFANYA MAONYESHO MAKUBWA YA BIASHARA NA UWEKEZAJI

 

Na Moses Ng'wat, Songwe.

Serikali mkoani Songwe imetangaza mpango kabambe wa kuanzisha maonyesho makubwa ya biashara na uwekezaji kuanzia mwaka 2026, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuongeza ushindani wa mkoa huo katika kuvutia wawekezaji na kupanua fursa za kiuchumi.

Hayo, yamebainishwa Novemba 28, 2025 na Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Jabiri omari Makame, wakati akifungua  mkutano wa tisa wa Baraza la Biashara la Mkoa uliofanyika katika ukumbi wa Chiku Galawa na kuhudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara na Viwanda, Dkt.Hashil Abdallah.

Makame, alisema maandalizi ya maonyesho hayo tayari yameingizwa kwenye mpango kazi wa serikali ya mkoa, yakihusisha sekta hizo za uwekezaji na biashara.

Alibainisha kuwa, tayari  serikali ya mkoa ilishaanza mchakato wa kuanzisha mpango wa maonyesho hayo na kwamba pendekezo lililotolewana wadau wa sekta binafsi kuhusu umuhimu wa jukwaa hilo limeungana na mawazo ya serikali ya mkoa, hivyo kuwataka wadau kujiandaa kushiriki kikamilifu.

Makame, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Biashara la Mkoa, alisema maonyesho hayo yatakuwa sehemu ya kukuza uelewa wa pamoja kati ya wawekezaji hasa katika sekta ya madini, wanunuzi na taasisi wezeshi, pamoja na kutoa nafasi ya kubadilishana uzoefu na kuonesha bidhaa na huduma.

“Serikali itaendelea kufanya kazi bega kwa bega na sekta binafsi ili kuchochea ukuaji wa uchumi katika mkoa wetu,” alisema Rc Makame.

Awali, Mwakilishi wa Chemba ya Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Kilimo (TCCIA) mkoani Songwe, Simon Kitojo, akitoa salamu za chemba hiyo,  alishauri mkoa wa Songwe kuwa na  maonyesho  yatakayokuwa yakihusisha wadau wa sekta za uwekezaji na biashara ili kuwa kichocheo cha kuongeza ushirikiano baina ya wadau, sanjari na kuvutia mitaji mipya kupitia uoneshaji wa bidhaa, ubunifu na fursa za uwekezaji.

Aidha, Kitojo aliwasilisha malalamiko ya wawekezaji katika sekta ya elimu, kuhusu mlundikano wa tozo kwenye biashara hiyo, ikiwemo kutozwa ushuru kwenye mazao kama mahindi waliyozalisha kwa ajili ya chakula cha wanafunzi.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Abdallah, alisema serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuboresha mazingira ya biashara kwa kutatua changamoto za wawekezaji na kuweka mifumo rafiki ya kuharakisha ukuaji wa uchumi.


Dkt. Hashil alisema Wizara ya Viwanda na Biashara imejipanga kuwafikia Wafanyabiashara popote walipo na kushughulikia changamoto zao kwa usahihi, haraka na kwa ufanisi.

"Sekta binafsi ikiwa ndio kichocheo cha maendeleo wanapaswa kufuatwa popote walipo na kusikilizwa na kutatuliwa changamoto zao" Dkt. Hashil alisema hayo, alipokuwa anazungumza na wajumbe wa Baraza la Biashara la Mkoa wa Songwe.


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI