Ghasia, vurugu na uharibifu mkubwa uliofanywa na magenge ya Vijana hapo Oktoba 29, 2025, umewaacha wananchi wa Mkoa wa Mwanza kukosa huduma muhimu za kijamii, huku pia mamia ya wananchi wakikosa ajira na kipato kutokana na matukio ya moto na wizi ulioangamiza maeneo yao ya kazi katika Eneo la Buhongwa Mkoani humo.
Kwa nyakati tofauti, magenge ya Vijana katika siku ya uchaguzi Mkuu wa Jumatano Oktoba 29, 2025, wakati wengine wakipiga kura kuwachagua Viongozi wao watakaowaongoza kwa miaka mitano ijayo, wao walivamia, kuiba na kuchoma moto Chuo cha Ufundi stadi VETA cha Buhongwa Mkoani Mwanza pamoja na kuiba na kuteketeza kwa moto Vituo vya uuzaji mafuta vya Olypic Petrol na Lake Oil Energies pamoja na kituo cha uuzaji wa bidhaa mbalimbali cha Empire store Kilichopo Igoma sambamba na magari yaliyokuwa yamepaki kwenye maeneo hayo.
Aidha wahalifu hao pia kando ya kuiba na kuteketeza kwa moto Ofisi ya Mtendaji wa Kata ya Buhongwa Mkoani humo, waliiba mali na samani mbalimbali za Ofisi pamoja na kuteketeza kituo cha Polisi Buhongwa, Kiwanda cha magodoro cha Super Banco na Kiwanda cha Vita Foam mkoani humo, suala ambalo limetajwa kuwaacha mamia ya Vijana na wananchi wa Mkoa huo na Mikoa ya jirani kukosa huduma mbalimbali na zaidi ajira kutokana na uharibifu huo mkubwa.





0 Comments