Header Ads Widget

'KESI YA LISSU YAAHIRISHWA SABABU ZA KIUSALAMA'- MWANASHERIA

 

Kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, (CHADEMA), Tundu Lissu, ambayo ilitarajiwa kuendelea leo Jumatatu, Novemba 10, 2025, imeahirishwa hadi Jumatano ya Novemba 12, ambapo itatajwa tena mahakamani.

Awali, upande wa Jamhuri ulipanga kuwasilisha shahidi wa nne katika kesi hiyo, lakini hilo halikuwezekana kutokana na hali ya sintofahamu iliyoibuka katika maeneo mbalimbali ya Tanzania kufuatia maandamano ya siku tatu yaliyoanza Oktoba 29, 2025. Mashahidi wanaotoka mikoa ya Ruvuma na Mbeya wameshindwa kusafiri kufika jijini kutokana na changamoto hizo za kiusalama.

Kwa mujibu wa maelezo ya upande wa mashtaka, hali hiyo imeathiri mchakato wa mashahidi kufika, na hivyo kufanya kesi ishindwe kuendelea kama ilivyopangwa. Wakili wa Serikali Mkuu, Thawabu Issa, aliieleza Mahakama kuwa ombi la kuahirisha linatolewa chini ya kifungu cha 302(a) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, Sura ya 20 (Toleo la 2023), akibainisha kuwa mashahidi wameshindwa kufika kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wao.

Kwa upande wa Jamhuri uliomba kesi iahirishwe kwa siku 14, Jaji Danstan Ndunguru aliamua ihahirishwe kwa siku mbili na kwamba shauri hilo litaendelea Jumatano ijayo badala ya muda huo mrefu uliotakiwa.

Wakili wa Lissu, Rugemeleza Nshalla, aliyeeleza kuhusu kuhairishwa kwa sababu ya usalama amesema wao wameweza kufika Mahakamani maana yake hali inaruhusu wengine kufika Mahakamani.

"Na tunafahamu kuwa mashahidi wengine ni wale wa kufichwa hata sijui usalama wao unahatarishwa vipi”, alihoji Nshalla na kuongeza, “Bahati mbaya mwenyekiti anajiwakilisha mwenyewe, hivyo hakuweza kuzungumza, tunatumaini kwamba umma ungependa kujua nini kinaendelea”.

Hata hivyo mwishoni mwa wiki, Makamu wa Rais, Dk Emmanuel Nchimbi, akizungumza kwenye mkutano wa nchi wanachama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kwamba hali ya nchi iko shwari.

"Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imechukua hatua za kurejesha utengemano katika nchi yetu ambao sasa nchi yetu (hali) ni shwari, na kila mtu anafuata utawala wa sheria", alisema Dk Nchimbi.

MWISHO.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI