Header Ads Widget

COPRA YATOA MAFUNZO KWA VIJANA ZAIDI YA 50 KWENDA KUWAINUA WAKULIMA WA ZAO LA PARACHICHI..

 

Na Matukio Daima Media.

Iringa.

Vijana 50 kutoka mradi wa Jenga Kesho iliyobora (BBT) ambao ni wahitimu wa taaluma ya kilimo kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine pamoja na vyuo vingine vya kilimo nchini wamepatiwa mafunzo elekezi ili kuwasaidia wakulima wa Parachichi kulima kwa ubora na kuachana na kilimo mazoea. 

Mafunzo hayo ya siku tatu yameanza leo mkoani Iringa na yanatolewa kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, lengo likiwa ni kuwasaidia wakulima kuleta tija katika zao la parachichi na kupata masoko.

Akifungua mafunzo hayo kwa njia ya Zoom, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA), Irene Madeje Mlola alisema kuwa mafunzo hayo yamelenga kuongeza ufanisi na kukuza mnyororo wa thamani katika uzalishaji wa mazao ya parachichi.

"Lengo ni kuhakikisha haya mazao mchanganyiko yanapata usimamizi ambao utaleta maendeleo kuanzia kwenye upande wa uzalishaji wenye tija mpaka kuhakikisha masoko yanapatikana," alisema Stella.

Aidha,  aliwataka vijana hao kuhakikisha wanawasimamia wakulima kuanza na kilimo chenye tija kwa kutumia kanuni bora za kilimo ili kuhakikisha kipato cha wakulima kimeongezeka.

Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Sehemu ya Mazao ya Bustani na Pareto kutoka COPRA, Lilian Mpinga, amesema kuwa lengo la kutoa mafunzo hayo ni kuongeza huduma za ugani hasa katika zao la parachichi.

Mpinga alisema kuwa vijana hao wamepata fursa kupitia programu ya BBT (Building Better Tomorrow) ugani, ambapo wataenda kutoa huduma za ugani katika maeneo mbalimbali ya kilimo cha parachichi.

"Mafunzo hayo elekezi yanalenga kuwapa ufahamu na uelewa wa taasisi ya COPRA namna inavyofanya kazi pamoja na kuelewa kazi wanayoenda kufanya wakiwa wanatoa huduma za ugani katika maeneo yao," alisema Kapinga.

Naye mmoja wa vijana wanaopata mafunzo hayo, Innocent Swai, mkazi wa Morogoro, alisema kuwa mafunzo hayo yamelenga kuboresha kilimo cha parachichi.


"Katika nchi yetu ya Tanzania, kilimo kinachangia kwa kiasi kikubwa katika uchumi wetu. Kwa hivyo, kupitia mradi huu wa BBT, kwa kushirikiana na Taasisi ya COPRA, tunatarajia kuibadilisha jamii kutoka katika kilimo cha mazoea na kuhamia kwenye kilimo chenye tija pamoja na kutafuta masoko," alisema Swai.

Afisa Ugani kutoka Mkoa wa Rukwa, Hamis Mwiga, alisema kuwa kupitia mafunzo hayo amejifunza jinsi ya kuongeza mnyororo wa thamani ili kujiongezea kipato na atahakikisha anaenda kuwasaidia wakulima katika mkoa wake.

Mwisho.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI