Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Kanda ya Pwani na Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, Boniface Jacob (Boni Yai), amekamatwa na Jeshi la Polisi leo Jumamosi, Novemba 8, 2025, akiwa njiani kuelekea Kituo cha Polisi Goba, jijini Dar es Salaam, kwa ajili ya kuripoti.
Taarifa za kukamatwa kwake zimethibitishwa na Wakili Hekima Mwasipu, ambaye amesema kuwa kiongozi huyo wa upinzani, ambaye pia ni Meya wa zamani wa Manispaa za Kinondoni na Ubungo, yupo mikononi mwa Polisi kwa mahojiano.
Kukamatwa kwa Jacob kunakuja saa chache baada ya Jeshi la Polisi, kupitia kwa Msemaji wake, kutangaza orodha ya watu 10 wanaosakwa kufuatia uchunguzi unaohusiana na matukio ya vurugu, uporaji wa mali na uvunjifu wa amani yaliyotokea Oktoba 29, 2025, katika maeneo mbalimbali nchini.
Miongoni mwa waliotajwa kwenye orodha hiyo ni viongozi kadhaa waandamizi wa CHADEMA, akiwemo Katibu Mkuu John Mnyika, Naibu Katibu Mkuu Tanzania Bara Amani Golugwa (ambaye alikamatwa mapema leo), Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi Brenda Jonas Rupia, Mjumbe wa Kamati Kuu Godbless Lema, Mwenyekiti wa BAVICHA Taifa Wakili Deogratias Mahinyila, na Mjumbe wa Baraza Kuu Hilda Newton.
Wengine waliotajwa ni Askofu Machumu Maximilian Kadutu (Askofu Mwanamapinduzi), ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima na pia Kada wa CHADEMA, pamoja na Askofu Josephat Gwajima, Mkuu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (MNEC).
Kwa mujibu wa taarifa ya Polisi, wote waliotajwa wametakiwa kujisilimisha mara moja katika vituo vya Polisi walipo karibu, pindi wanapoona taarifa hiyo.

.jpg)




0 Comments