Waasi wanaodhibiti migodi ya dhahabu ya kampuni ya Twangiza mashariki mwa Jamhuri mwa Kidemokrasi ya Congo wamepora takriban kilo 500 za dhahabu tangu mwezi Mei.
Kampuni hiyo imewashutumu baadhi ya wafanyakazi wake kwa kuchangia katika wizi huo wa dhahabu.
Thamani ya dhahabu hiyo iliyoibwa ni karibu dola milioni 70.
Mgodi huo wa kampuni ya Twangiza uko jimboni Kivu Kusini ambako waasi wa M23 waliyateka na kuyadhibiti maeneo mengi ya jimbo hilo ikiwemo mgodi huo.
Taarifa inasema baadhi ya wafanyakazi wa kampuni hiyo walisaidia katika kusafirisha shehena ya kwanza ya zaidi ya kilo 50 ya dhahabu na kuongeza kuwa tangu waasi wa M23 walipochukua udhibiti wa eneo hilo, wamepoteza kiasi cha kilo 500 za dhahabu zinazosafirishwa kisirisiri kupitia njia za chini ya ardhi.
Mbali na madini hayo kuibiwa, kampuni hiyo ya Twangiza yenye makao yake makuu nchini DR Congo inayojitambulisha kuwa kampuni ya kichina inasema pia imepoteza vifaa vya thamani ya dola milioni 5.
Twangiza imesema inapanga kuwasilisha malalamishi rasmi kwa serikali ya DRC na asasi nyingine za kimataifa kusuluhisha tatizo hilo.
Aidha inawashutumu waasi kwa kuwafurusha wakaazi, kuyabomoa makanisa na kutumia wataalam wa kiufundi wa Rwanda kupata data za kijielojia na kutanua shughuli za uchimbaji madini.
M23 haijazungumzia shutuma hizo.
Serikali ya Rwanda amabyo mara kwa mara imekuwa ikikanusha kuhusika katika mzozo wa mashariki mwa Congo na kuwaunga mkono waasi wa M23 pia haijatoa tamko lolote kuhusiana na madai hayo.
0 Comments