Iwapo mateka na wafungwa wa pande zote mbili watabadilishana kwa mafanikio, inaaminiwa kuwa mazungumzo yatafuata kuhusu awamu za mwisho za mpango wa vipengele 20 uliowasilishwa na Trump.
Mpango huo wa kusitisha mapigano Gaza unabainisha kuwa iwapo utakubaliwa na pande zote mbili, vita vitasitishwa mara moja.
Aidha mpango huo pia unapendekeza kuwa Ukanda wa Gaza uvuliwe silaha, na miundombinu yote ya kijeshi, ya kigaidi na ile ya mashambulizi iharibiwa kabisa.
Katika awamu ya mpito, Gaza itatawaliwa na kamati ya muda ya wataalamu wa Kipalestina (technocrats), chini ya usimamizi wa “Bodi ya Amani” itakayoongozwa na Donald Trump, kwa ushirikiano na Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, Tony Blair.
Hatimaye, mamlaka ya kuongoza Gaza yatakabidhiwa kwa Mamlaka ya Palestina ambayo kwa sasa inasimamia Ukingo wa Magharibi baada ya kupitia mageuzi ya kimuundo.
Kulingana na mpango huo, Hamas ambayo imetawala Ukanda wa Gaza tangu mwaka 2007 haitakuwa na nafasi yoyote katika uongozi wa baada ya vita, iwe kwa njia ya moja kwa moja au isiyo ya moja kwa moja.
Wanachama wa Hamas watapewa msamaha endapo watakubali kuishi kwa amani, au watapatiwa njia salama ya kuhamia nchi nyingine.
Hakuna Mpalesitina atakayelazimishwa kuondoka Gaza, na wale watakaotaka kuondoka watakuwa na haki ya kurejea.
Mpango wa kiuchumi wa Trump wa kuijenga upya na kuhuisha Gaza utaundwa na jopo maalum la wataalamu wa maendeleo.
Hata hivyo, Hamas imekuwa ikikataa kuweka silaha chini, ikisisitiza kuwa itafanya hivyo tu baada ya kuanzishwa kwa taifa huru la Palestina.
Aidha, katika majibu yake ya awali kwa mpango huu mwishoni mwa wiki iliyopita, Hamas haikutaja chochote kuhusu suala la kusalimisha silaha, jambo lililozua hisia kuwa msimamo wake bado haujabadilika.
Ingawa Israel imekubali mpango wa Trump kwa ujumla wake, Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu alionekana kupinga ushiriki wa Mamlaka ya Palestina katika Gaza ya baada ya vita, licha ya kusimama jukwaa moja na Rais wa mamlaka hiyo wiki iliyopita.
Kwa upande wake, Hamas imesema inatarajia kuwa na nafasi katika mustakabali wa Gaza, ikiwa kama sehemu ya “harakati moja iliyounganisha Wapalestina”.
Naye Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya, Kaya Kallas, alisema kuwa ujumbe wa ufuatiliaji wa kiraia katika kivuko cha mpaka cha Rafah kati ya Ukanda wa Gaza na Misri utaanza tena shughuli zake siku ya Jumatano, akibainisha kuwa ingawa kupatikana kwa amani Gaza bado ni "changamoto sana," ujumbe wa ufuatiliaji unaweza kuchukua "jukumu muhimu" katika kusaidia utulivu wa usitishaji mapigano.
Swali lingine linalozua mjadala ni kuhusu kiwango cha uondoaji wa majeshi ya Israel.
Israel imesema kuwa katika hatua ya awali ya kujiondoa, itaendelea kudhibiti takriban asilimia 53% ya Gaza.
Mpango wa Ikulu ya Marekani unaonesha hatua za ziada za kujiondoa hadi kufikia 40%, na hatimaye 15%.
Awamu ya mwisho ya uondoaji huo itaweka “eneo la usalama” ambalo litaendelea kudhibitiwa hadi Gaza itakapothibitishwa kuwa salama dhidi ya tishio lolote jipya la ugaidi.
Hata hivyo, maelezo haya ni ya jumla na hayatoi ratiba maalum ya kuondoka kikamilifu kwa majeshi ya Israel jambo ambalo huenda likawa moja ya mada kuu zitakazoshinikizwa na Hamas katika mazungumzo yajayo.
0 Comments