Na Matukio Daima Media
Iringa
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, amepongeza na kuyataka mashirika yanayotekeleza miradi ya maendeleo inayolenga kumuinua mtoto wa kike kuendelea kufanya kazi kwa weledi, uwazi na uadilifu ili kuchangia maendeleo ya jamii.
Akiyasifu Shirika la Rural Development Organization (RDO) na Brac Tanzania, RC Kheri alisema mchango wa mashirika hayo umeleta mabadiliko chanya katika kuinua elimu, afya na ustawi wa wasichana mkoani Iringa.
Akizungumza kwenye kilele cha Siku ya Mtoto wa Kike Duniani kilichofanyika katika Viwanja vya Mwembetogwa, Manispaa ya Iringa, Mkuu wa Mkoa alisema kuwa serikali inatambua na kuthamini juhudi za mashirika yanayochochea fursa na usawa kwa mtoto wa kike, hasa kwenye maeneo ya vijijini ambako bado kuna changamoto za ukatili, ndoa za utotoni na mimba za mashuleni.
“Ninawapongeza RDO, Brac Tanzania na wadau wengine kwa kazi kubwa mnayoifanya ya kumsaidia mtoto wa kike. Nitoe wito kwa mashirika yote yaliyosajiliwa kufanya kazi za kijamii kuhakikisha yanatekeleza majukumu yao kulingana na maombi ya usajili wao na si vinginevyo,” alisema RC Kheri.
Aliongeza kuwa Mkoa wa Iringa unatarajia kufanya uhakiki wa mashirika yote yasiyo ya kiserikali (NGOs) ili kuhakikisha yanafanya kazi kwa tija na kwa mujibu wa sheria.
RDO Waendelea Kuwainua Wasichana Kiuchumi na Kielimu
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mkurugenzi wa Shirika la RDO, Fidelis Filipatali, alisema shirika hilo limekuwa mstari wa mbele kupambana na changamoto zinazomkabili mtoto wa kike kwa vitendo. Kupitia vyuo vyake vya ufundi stadi vilivyopo Mdabulo, Kilolo na Mafinga, RDO imewezesha mamia ya wasichana kupata elimu ya ufundi pamoja na ujuzi wa kujitegemea.
“Tunatoa mafunzo ya ufundi stadi kama ushonaji, umeme wa majumbani, useremala, ufundi pikipiki pamoja na TEHAMA lengo ni kumjenga mtoto wa kike awe na uwezo wa kujitegemea na kuondokana na utegemezi unaosababisha unyanyasaji,” alisema.
Filipatali aliongeza kuwa kupitia programu za RDO, wasichana waliokosa fursa ya kuendelea na masomo kutokana na changamoto za kifamilia au mimba za utotoni wamepata nafasi ya pili ya kuandika maisha yao upya.
Umuhimu wa Siku ya Mtoto wa Kike Duniani
Siku ya Mtoto wa Kike Duniani huadhimishwa kila mwaka Oktoba 11, kwa lengo la Kupaza sauti dhidi ya ukatili wa kijinsia unaomkabili mtoto wa kike Kupambana na ndoa na mimba za utotoni,Kutetea haki ya mtoto wa kike kupata elimu bora,Kufungua fursa za usawa katika uongozi na uchumi, Kulinda afya ya mtoto wa kike ikiwemo afya ya uzazi na Kuhamasisha jamii kumlinda na kumthamini mtoto wa kike
Shirika la Umoja wa Mataifa (UN) linaeleza kuwa mtoto wa kike anapaswa kupewa ulinzi na fursa sawa na wavulana ili kufikia malengo ya maendeleo endelevu (SDGs), hususan malengo ya kupunguza umaskini, ubora wa elimu na usawa wa kijinsia.
Changamoto Zinazoendelea Kumkabili Mtoto wa Kike
Licha ya hatua zilizopigwa, bado kuna changamoto zinazowakabili wasichana nchini, ikiwemo:
- Ndoa za utotoni
- Mimba za shuleni
- Ukatili wa kijinsia (GBV)
- Ukatili wa kisaikolojia na kingono
- Utoro na utoro sugu shuleni
- Umaskini na ukosefu wa mahitaji ya msingi kama taulo za kike
- Mila na desturi kandamizi
- Ajira za utotoni
Katika maadhimisho hayo, wadau wa haki za watoto waliitaka jamii Wazazi wawalee watoto katika misingi ya maadili na ulinzi, Jamii ishirikiane kuzuia ukatili dhidi ya mtoto wa kike, Mamlaka zichukue hatua kali kwa wanaohusika na ndoa na mimba za utotoni,Mashirika yaendelee kutoa elimu na uhamasishaji vijijini na Wasichana wajiamini na kuthubutu kutimiza ndoto zao
0 Comments