MGOMBEA Udiwani katika kata ya Isamilo, Wilaya ya Nyamagana, Mkoani Mwanza, kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Charles Nyamasiriri akinadi sera kwenye Mkutano wa kampeni.NA CHAUSIKU SAID, MATUKIO DAIMA MWANZA.
MGOMBEA Udiwani katika kata ya Isamilo, Wilaya ya Nyamagana, Mkoani Mwanza, kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Charles Nyamasiriri, ameahidi kushirikiana na wananchi wa kata hiyo kuendeleza miradi ya maendeleo na kutatua changamoto zilizobakia.
Akizungumza hayo jana Oktoba 24, mwaka huu, katika viwanja vya Mwembeni wakati akihitimisha kampeni za uchaguzi na kuomba ridhaa ya kuchaguliwa kuwa diwani kata hiyo na kueleza kuwa lengo lake ni kuhakikisha maendeleo yanapatikana katika kata hiyo ili kukamilisha Miradi ambayo haikukamilika Kwa kushirikiana na wananchi Kwa miaka 5 mingine.
"Nitalia na nyie Wanaisamilo, lengo ni kuhakikisha nakwenda kuleta maendeleo na kuendelea na ushirikiano ulio mkubwa," alisema Nyamasiriri.
Nyamasiriri amesema kuwa kwa kushirikiana na serikali ya awamu ya sita, tayari kuna mafanikio katika miundombinu ya barabara, zahanati, na huduma nyingine muhimu, na kutaja barabara inayotoka Makondeko imejegwa na kubakia kipande cha mita 120 ili iweze kukamilika.
"Barabara hii itakamilika hivi karibuni kwani mkandarasi amesaini mkataba na kazi inaendelea, Pia, barabara ya kutoka kuelekea Olenjolai Sekondari inahitaji kumaliziwa," alisema Nyamasiriri.
Nyamasiriri ameeleza kuwa serikali ya awamu ya sita imefanya kazi kubwa katika kuboresha miundombinu ya barabara, hivyo ataendelea na juhudi hizo kwa kushirikiana na wananchi wa kata hiyo, huku akitoa mfano wa barabara inayotoka Makondeko kujengwa na kutoa huduma bora kwa wananchi.
"Pia, kuna kile kipande cha barabara ya Genge la washashi kilichobakia tayari mkandarasi amesaini mkataba na muda sio mrefu, kipande hicho kitakamilika," alisema Nyamasiriri.
Nyamasiriri pia alieleza kwamba serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imeleta fedha nyingi kwa ajili ya miradi ya maendeleo katika kata ya Isamilo, na kwa kushirikiana na mgombea ubunge wa Nzilanyingi, miradi hiyo itakamilika kwa wakati.
"Zaidi ya milioni 3.2 zimetumika kwa ajili ya miradi ya barabara na zahanati. Tumefanya kazi kubwa kuhakikisha huduma hizi zinapatikana kwa kila mwananchi wa kata ya Isamilo," alifafanua Nyamasiriri.
Nyamasiriri aliwahimiza wananchi kumchagua ili aweze kuendelea kutekeleza miradi hiyo ya maendeleo kwa manufaa ya wote.
"Nipeni kura zenu, niendelee kufanya kazi kwa ushirikiano na nyie Wanaisamilo ili tuendelee na mwelekeo mzuri wa maendeleo," alisema Nyamasiriri.
Mwisho.









0 Comments