Na COSTANTINE MATHIAS, Itilima.
MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Itilima kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Njalu Daudi Silanga, ameendelea na kampeni zake huki akihimiza wananchi kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura Oktoba 29, kumchagua Dkt. Samia Suluhu Hassan ili awe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Njalu pia amewataka wananchi hao kumpigia kura za ndiyo ili aweze kuwa Mbunge na mwakilishi wa wananchi Bungeni pia kuwachagua madiwani wote wanaotokana na CCM.
Akizungumza kwa nyakati tofauti katika mikutano ya hadhara iliyofanyika katika Vijiji vya Nyantugutu, Mwamalinze, Gaswa na Mwabuki wilayani Itilima, Njali amewataka wananchi wa Itilima kudumisha mshikamano, amani na upendo walionao.
“Leo Itilima tunajivunia tulipo kwa sababu ya mshikamano wetu, nawaomba ndugu zangu tuilinde amani na umoja huu ili siku ya Oktoba 29 tujitokeze kwa pamoja tukaichague CCM kuanzia kwa Rais Samia, mama ambaye utendaji wake si wa kutiliwa mashaka... Pia mkanipe kura ya ndiyo ili tuendelee kuijenga Itilima yetu, msisahau pia kuwapigia kura madiwani wetu wa CCM,” amesema Silanga.
Ameongeza kuwa maendeleo yaliyopatikana katika awamu ya sita ni kielelezo cha dhamira ya kweli ya CCM katika kuboresha maisha ya wananchi. Hivyo akasisitiza kuwa ni jukumu la kila mwananchi wa Itilima kuhakikisha wanashiriki ipasavyo katika uchaguzi huo ili kuimarisha uongozi wa chama hicho.
Mwisho.












0 Comments