Header Ads Widget

MISS WORLD CHINA ATEMBELEA HIFADHI YA MAKUYUNI WILDLIFE PARK


Hifadhi ya Makuyuni Wildlife Park, iliyopo takribani kilomita 70 kutoka Jiji la Arusha, imeendelea kung’ara katika kurasa mbalimbali za habari za utalii duniani baada ya kupokea ugeni mzito wa Miss World China 2021 Bi Jiang Sigi, aliyefika hifadhini hapo leo Oktoba 11, 2025 akiwa ameambatana na washindi wa tuzo ya Miss Travel kutoka Hong Kong - China, Kenya na Tanzania.

Ziara hiyo maalum ya siku moja, iliyoratibiwa na kampuni ya Miss Travel World Beauty Pageant T/A Skyvfree International) chini ya kampuni mama Goshen Safaris, imelenga kuwapa wageni hao wenye ushawishi mkubwa katika nchi zao fursa ya kushuhudia vivutio vya utalii vilivyopo Makuyuni, na Kupitia majukwaa yao ya kimataifa, wageni hao wanatarajiwa kusaidia kuitangaza kwa kuionesha dunia jinsi Makuyuni Wildlife Park inavyozidi kuwa kivutio cha Kimataifa cha utalii wa wanyamapori, mandhari na utamaduni wa asili.

Akizungumza mara baada ya ziara hiyo, Mkurugenzi Mratibu wa Miss  Travel World - Tanzania, Samweli Mulugu alisema kuwa hatua hiyo ni sehemu ya jitihada endelevu za kukuza utalii wa Tanzania kupitia wageni mashuhuri wenye ushawishi mkubwa katika nchi zao. Aliongeza kuwa kupitia ugeni huo, Hifadhi ya Makuyuni Wildlife Park itaendelea kujulikana zaidi katika soko la kimataifa na kuvutia wawekezaji wa sekta ya utalii.


Aidha, alitoa pongezi kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kwa juhudi zake katika kuendeleza utalii endelevu, kuhifadhi urithi wa asili, na kulinda tamaduni za jamii jirani.

Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi  wa Uhifadhi anayesimamia utalii – Kanda ya Kaskazini,  Segoline Tarimo, aliishukuru kampuni ya Goshen Safaris kwa kuunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kutangaza vivutio vya utalii vya nchi yetu kupitia filamu  za Tanzania The Royal Tour na Amazing Tanzania.

Pia alitumia nafasi hiyo kuwakaribisha wageni kutoka ndani na nje ya nchi kutembelea Hifadhi hiyo ili waweze kujionea vivutio mbalimbali vya utalii.


Wakati wa ziara hiyo, wageni walipata fursa ya kujionea wanyamapori mbalimbali mubashara wakiwemo tembo, twiga, swalapala, choroa (oryx), pundamilia na wengine wengi, sambamba na burudani za ngoma za jadi za Kimasai.

Kutokana na kuvutiwa na mandhari na vivutio vya hifadhi hiyo, wageni hao walieleza azma yao ya kurejea tena Makuyuni Wildlife Park kwa ajili ya kufanya utalii wa kupanda vilima (hiking) na kuendelea kutangaza vivutio vya Tanzania kwa dunia.





Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI