Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI anayeshughulikia Miundombinu, Mhandisi Rogatus Mativila ametembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa barabara ya Utete-Kingupira yenye urefu wa Kilomita 32 inayojengwa kwa kutumia Teknolojia Mbadala ya “Eco-roads” wilayani Rufiji mkoani Pwani.
Akizungumza baada ya kukagua mradi huo, Mhandisi Mativila amesema kuwa, katika barabara hiyo Kilomita 2 itawekwa lami na sehemu inayobakia itawekwa changarawe huku akimtaka Mkandarasi RAPCO Construction Company kukamilisha kazi hiyo kwa wakati kabla mvua hazijaanza.
“Nina imani na Mkandarasi huyu kwani amefanya vizuri katika mradi mwingine wa barabara ya Chumbi-Kiegele, utekelezaji wa kazi hii umefika asilimia 40, nina amini kazi hii nayo ataikamilisha kwa wakati, maelekezo ni kwamba Mkandaradi aikimbize kazi hii kabla mvua hazijaanza ili ikamilike kwa wakati”, amesema.
Aidha, amemtaka Meneja wa TARURA mkoa wa Pwani kusimamia mradi huo ili ukamilike kwa wakati kwani barabara hiyo ni muhimu kwa usafirishaji wa mazao mbalimbali.
Akisoma taarifa ya mradi, Meneja wa TARURA wilaya ya Rufiji, Mhandisi Nicholaus Ludigery amesema kuwa mradi huo wenye thamani ya Shilingi Bilioni 2.5 ni muhimu kwa wana Utete na wana Rufiji kwa ujumla kwani barabara hiyo inaelekea kwenye hifadhi ya Taifa ya Selous na wananchi wanafanya shughuli za kilimo cha ufuta, korosho, machungwa na mazao mengine mbalimbali.
Ameongeza kuwa kukamilika kwa barabara hiyo itarahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji, itarahisisha kuzifikia huduma za kijamii na pia wakulima wataweza kusafirisha mazao yao sokoni kwa urahisi.
0 Comments