Baadhi ya washiriki wa Tamasha la Michezo na Afya lililofanyika leo katika viwanja vya Jiji vilivyopo Ngarenaro,Arusha
Na, Egidia Vedasto,
Matukio Daima, Arusha.
Katika bonanza la afya na michezo lililoandaliwa na klabu ya jogging Jijini Arusha na kufanyika katika viwanja vya Ngarenaro, jamii imekumbushwa kufanya mazoezi mara kwa mara ili kukabiliana na magonjwa tishio yanayoikabili jamii kwa wingi.
Akizungumza na wananchi walioshiriki bonanza hilo Mganga mkuu wa mkoa Dr.Charles Rashid Mkombachepa amesema si lazima kufanya mazoezi uwanjani bali yanaweza kufanyika hata chumbani hatua inayoweza kuepusha gharama za matibabu zisizo za lazima.
"Kiwango cha matibabu ya Dialysis kwa maramoja si chini ya shilingi laki mbili, na inawezekana tatizo hili linazidi kuwa kubwa kwa sababu ya watu kutopenda kufanya mazoezi. Nawasihi wananchi kupenda kufanya mazoezi kama wanamvyopenda kula ili kuokoa fedha nyingi kwa ajiki ya matibabu"amesema.
Hatahivyo Dr. Mkombachepa amewakumbusha wananchi kudumisha amani na utulivu katika kipindi hiki nchi inapoelekea katika uchaguzi mkuu Oktoba 29."Uchaguzi ni haki ya kila mtu kumchagua kiongozi bora kwa maendeleo yetu".
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi Mkoa wa Arusha (APC) Claud Gwandu amesema mazoezi ni afya kila mmoja anapaswa kujali afya yake.
"Kipekee napongeza Klabu ya Jogging mkoa wa Arusha, Mganga mkuu wa mkoa wa Arusha, na wadau wote walioshiriki katika bonanza hili, tuendelee kufanya mazoezi maana afya ni mtaji" amesema.
Katika namna hiyo hiyo Katibu wa chama cha waendesha pikipiki Jijini Arusha Richard Magembe amesema mazoezi kwake ni desturi na yamemsaidia sana kuweka mwili wake sawa.
"Kazi yangu inanitaka kuwa na afya njema mwenye stamina ya kubeba vitu vizito. Naomba utaratibu huu uwe endelevu makundi mbalimbali yahamasishwe kushiriki mazoezi"amesema.
Vile vile Mmoja wa vijana walioshiriki bonanza hilo Grace Tarimo amesema mazoezi ndio njia pekee ya kuepuka na magonjwa yasiyoambukiza kama shinikizo la damu, uzito uliopitiliza na sukari.
"Napenda kufanya mazoezi kila wakati na yamenisaidia sana kuwa na pumzi, afya njema, na wepesi katika kutekeleza shughuli zangu, nawakumbusha vijana wenzangu kutumia ipasavyo haki yao ya msingi kupiga kura kuwachagua viongozi bora wakati utakapowadia" amesema.
Bonanza hilo limepambwa na michezo mbali mbali ikiwemo mashindano ya kukimbia, mpira wa wavu na kikapu, karate na zawadi mbalimbali kutolewa kwa walioibuka washindi. Wanafunzi wa shule ya Arusha sekondari wameibuka kidedea katika mchezo wa wavu na kujinyakulia zawadi ya kikombe cha dhahabu.
Mwisho.
0 Comments