
Na COSTANTINE MATHIAS, Bariadi.
MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Bariadi Mjini, kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mhandisi Kundo Mathew amesema kuwa endapo atachaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo hilo, atahakikisha anaisimamia serikali kujenga daraja la Mto Bariadi linalounganisha mitaa wa Ditima na Yeya, iliyopo kata ya Guduwi ili kufungua fursa ya Uchumi na kurahisisha mawasiliano, usafiri na usafirishaji.
Mhandisi Kundo amesema kuwa endapo ujenzi wa daraja hilo utakamilika, utafungua fursa ya Biashara ya mazao, usafiri na usafirishaji hasa nyakati za masika na pia wananchi wataondokana na adha ya kusombwa na Maji au kupoteza maisha.
Akizungumza kwenye Mkutano wa kampeni uliofanyika mtaa wa Ditima, Mhandisi Kundo amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi Oktoba 29, 2025 kumchagua Mgombea Urais Dk. Samia Suluhu Hassan, Mgombea Ubunge (Mhandisi Kundo) na Diwani wa CCM ili washirikiane kuondoa adha hiyo iliyokuwa inawakabili wananchi kwa muda mrefu.
"Kiu yangu ni kujenga na kukamilisha daraja la Ditima kwenda Yeya ili kufuingua Bariadi kimawasiliano na kurahisisha usafiri...Wafanyabiashara watapitisha mazao yao kutoka Ngulyati kupita Guduwi kwenda Bariadi na Dutwa, Kiunganishi hapa ni kujenga daraja, tupeni kura CCM ili tumalize tatizo hili" Amesema Mhandisi Kundo.
Kuhusu changamoto ya Mtandao wa umeme, Mhandisi Kundo amesema kuwa agenda ya 2025, ilikuwa ni kufikishwa Umeme kwenye vijiji lakini sasa serikali imekuja kufanya ujazilishi kupitia Mradi wa Compact Mission 300 ambapo kila mwananchi kwenye Jimbo la Bariadi Mjini atafikiwa na Umeme.
Mwisho.
0 Comments