Header Ads Widget

MAKAMU WA RAIS ASHIRIKI JUBILEI YA MIAKA 50 YA DAYOSISI YA PARE*


ASISITIZA UMUHIMU WA KUENDELEA KULIOMBEA TAIFA NA KUFUNDISHA MAADILI MEMA KWA VIJANA

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa taasisi za dini kutambua wajibu wa kuendelea kusimama katika nafasi yake ya kuombea taifa, kufundisha imani ya kweli ya Mungu, kukemea maovu katika jamii, kufundisha maadili mema na kuwa kielelezo cha haki na uadilifu.

Makamu wa Rais ametoa wito huo mara baada ya kushiriki Ibada Maalum ya Jubilei ya Miaka 50 ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Pare, iliyofanyika Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro. Amesema kwa njia hiyo Kanisa litachangia katika kujenga jamii inayowajibika na yenye uadilifu. Aidha, amesema ni muhimu kuwa wabunifu na kutumia fursa ya maendeleo makubwa ya TEHAMA ikiwemo mitandao ya kijamii katika kuinjilisha na kutoa huduma nyingine muhimu.

Makamu wa Rais amewasihi wazazi, walezi, jamii na Kanisa kwa ujumla kupima faida na madhara ya TEHAMA na kuwajengea uwezo vijana kuhusu matumizi bora ya teknolojia ili yawe matumizi salama na yenye tija. Amesema ni vema kuhimiza mawasiliano ya ana kwa ana kati ya vijana, ikiwemo kuhimiza vijana washiriki vyama vya kufundisha maadili ya dini na mila na desturi njema kupitia michezo, sanaa, shughuli za kijamii na kidini ili kupunguza utegemezi wa kupitiliza kwenye mitandao.


Amesema ulimwengu wa kidijitali umeleta fursa nyingi kwa vijana, Kanisa  na Taifa kwa ujumla ikiwemo urahisi wa kujipatia elimu, kupashana habari ikijumuisha kutangaza neno la Mungu na kurahisisha mawasiliano kwa ujumla. Hata hivyo, ulimwengu huo wa kidijitali umeambatana na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na hatari kwa vijana kuathirika na maudhui hasi kama unyanyasaji mtandaoni, picha na video chafu, ujumbe wa kuchochea chuki, kuathirika kwa afya ya akili kutokana na utegemezi uliopitiliza kwenye mitandao, muziki masikioni na kupungua kwa mawasiliano ya moja kwa moja miongoni mwa jamii.

Vilevile, Makamu wa Rais amesema Pamoja na mafanikio makubwa yaliyofikiwa katika jitihada za kuinjilisha na kuboresha maisha ya watu, jamii bado inakabiliwa na changamoto nyingi za kijamii na kiroho, ambazo zinapaswa kuendelea kufanyiwa kazi kama vile mmomonyoko wa maadili, kuongezeka kwa vitendo vya ukatili na mauaji katika jamii pamoja na migogoro ya kifamilia inayopelekea kuvunjika kwa ndoa na kusababisha ongezeko la watoto wa mitaani.

Pia amesema changamoto zingine ni pamoja na mafundisho potofu, rushwa na ufisadi, matumizi mabaya ya pombe na mihadarati kama bangi na mirungi, vijana kutumia muda mwingi kubet, kucheza kamari  badala ya kupenda kufanya kazi, kuminywa kwa haki za watoto na wanawake, magonjwa ya afya ya akili na yale yasiyoambukizwa, pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi unaotokana na uharibifu wa mazingira.


Halikadhalika Makamu wa Rais, ametoa wito wa umuhimu wa kutunza mazingira na kuendelea kuchukua hatua za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi zinazosabishwa na uharibifu wa mazingira. Ameipongeza Dayosisi ya Pare kwa kutekeleza mradi wa utunzaji wa mazingira kupitia kilimo cha zao la parachichi, michungwa na miti ya asili kwa ushirikiano na Shirika la Forest Focus.

Makamu wa Rais amesema Serikali inajivunia ushirikiano mzuri uliopo kati yake na KKKT, na taasisi nyingine za dini, ambao umedumu kwa muda mrefu katika nyanja mbalimbali. Amesema pia, inatambua na kuthamini mchango mkubwa wa KKKT katika utoaji wa huduma za jamii, hususan elimu, afya na maji.

Makamu wa Rais amewasihi wana Dayosisi ya Pare pamoja na Watanzania kwa ujumla wenye sifa ya kupiga kura kujitokeza katika kupiga kura mwishoni mwa mwezi Oktoba, ili kutumia haki yao ya kidemokrasia kuwachagua viongozi wanaowataka. Aidha amesema ni muhimu kuendelea kudumisha hali ya amani na utulivu kote nchini kabla, wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu.

Akitoa mahubiri katika Ibada hiyo, Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dkt. Alex Malasusa ametoa wito kwa Watanzania kumshukuru Mungu kwa amani ambayo Taifa limejaaliwa. Amewasihi waumini kuhakikisha wanashiriki katika Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani na kuwa mabalozi wa amani, utulivu na ustahimilivu. Aidha ametoa wito kwa waumini kuendelea kuiombea Tanzania ili kuendelea kuwa Taifa lenye amani na utulivu.






 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI