Na Matukio Daima Media, Dodoma
Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kimetoa wito kwa walimu kote nchini kushiriki kikamilifu katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, sambamba na kutumia nafasi yao muhimu katika jamii kuelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kushiriki zoezi hilo la kidemokrasia.
Wito huo umetolewa na Rais wa CWT, Dkt. Selemani Ikomba, wakati wa Mkutano wa Ujirani Mwema wa Viongozi wa CWT kutoka Kanda ya Kaskazini na Kanda ya Kati uliofanyika hivi karibuni.
Dkt. Ikomba amesisitiza kuwa walimu si tu ni msingi wa elimu katika taifa, bali pia ni viongozi wa fikra na maadili ndani ya jamii, hivyo wana wajibu wa kuhamasisha ushiriki hai wa wananchi katika masuala ya kiraia kama uchaguzi.
"Uchaguzi ni njia ya amani na kidemokrasia ya kuchagua viongozi watakaowakilisha matakwa ya wananchi na kuleta maendeleo katika sekta mbalimbali, ikiwemo elimu," amesema Dkt. Ikomba.
Ameongeza kuwa kupitia ushiriki wao, walimu wanaweza kusaidia kupunguza changamoto zinazowakabili katika sekta ya elimu kama vile uhaba wa miundombinu, maslahi duni, na mazingira magumu ya kufundishia.
Aidha, amewataka walimu kutumia muda huu kuelimisha wanafunzi, wazazi, na jamii kwa ujumla kuhusu haki na wajibu wao wa kikatiba kushiriki katika uchaguzi, huku wakihimiza amani, mshikamano, na uzalendo katika kipindi hiki muhimu kwa taifa.
Dkt. Ikomba pia ametoa wito kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi na wadau wengine kuhakikisha kuwa mazingira ya uchaguzi ni salama, huru na haki ili kuwapa wananchi imani ya kushiriki bila woga au vikwazo.
Kwa ujumla, CWT inasisitiza kuwa ushiriki wa walimu katika mchakato wa uchaguzi si wa hiari tu, bali ni wajibu wa kitaaluma na kijamii unaochangia kuimarisha demokrasia, utawala bora, na maendeleo endelevu ya taifa.
0 Comments