BODI YA PAROLE YAPENDEKEZA KUACHIWA 163
NA MATUKIO DAIMA MEDIA
JESHI la Magereza limeeleza kuwa litahakikisha wafungwa wenye sifa za kisheria wanashiriki kupiga kura katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 29 mwaka huu, wa Rais, Wabunge na Madiwani Kwa maelekezo yote yanayoendelea kufanywa na Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi INEC.
Aidha wameendelea na utekelezaji wa maamuzi ya Bodi ya Parole Kwa kupendekeza kwa Waziri mwenye dhamana ya mambo ya ndani kuachiwa kwa wafungwa 163 wakiwemo wanawake 11.
Kamishna Jenerali wa Magereza, Jeremiah Katungu, amesema hatua hizo mbili zinadhihirisha dhamira ya Serikali kuendeleza haki za msingi za binadamu, ikiwemo haki ya kuchagua viongozi na kupata nafasi ya pili ya maisha kwa wafungwa wanaostahili.
CGP Katungu alisema wafungwa 163 wanaopendekezwa kuachiwa ni kati ya 206 wakiwemo wanawake 13 waliojadiliwa na bodi hiyo
"Wafungwa 43 wakiwemo wanawake wawili hawakupendekezwa kutokana na sababu mbalimbali licha ya kujadiliwa"Aliisitiza CGP ambaye ndiye katibu wa bodi ya Parole.
Kamishna huyo Jenerali wa Magereza alisema mfumo wa Parole una manufaa makubwa kwa taifa, ikiwemo kupunguza gharama za uendeshaji wa magereza, kuruhusu jamii kushiriki katika mchakato wa urejeshaji wa nidhamu, na kuimarisha mahusiano kati ya jamii na jeshi la magereza.
Aidha unafanya wafungwa kuungana tena na familia zao wakiwemo wake , waume, watoto, wazazi, Ndugu na jamaa na kuimarisha upendo na mahusiano na kuwapa fursa ya kujishughulisha na shughuli za maendeleo zinaazochangia ukuaji wao wa uchumi wa familia na Taifa Kwa ujumla.
"Kabla ya kupendekeza kuachiwa huwa tunaangalia tabia na mienendo yao wanapokuwa gerezani,utayari wa jamii kuwapokea,wawe wametumikia kifungo chao kwa moja ya tatu,lakini pia Aina ya makosa Yao Kwa mujibu wa Sheria" Aliongeza
Balozi Hamis Kagasheki, Mwenyekiti wa Bodi ya Parole, amesema jamii inapaswa kutambua kuwa mfumo wa Parole si tu njia ya kupunguza msongamano, bali ni chombo cha kurejesha utu, nidhamu na matumaini mapya kwa wale waliokwenda kinyume na sheria lakini wameonyesha mabadiliko chanya.
Akaiasa jamii kuwa tayari kuwapokea wafungwa hao wanaorudi kumalizia vifungo vyao kwenye jamii, kwani tayari wamerekebishika kwasababu wakiwa gerezani wanapata elimu na mafunzo tofauti na zamani enzi za ukoloni ambapo kifungo ilikuwa ni adhabu za kazi Ngumu na mateso pekee.
"Wameelimishwa namna ya kuishi na jamii,kuepuka mambo yanayoweza kuwatia hatiani na kurudishwa gerezani hivyo ni vyema wananchi waelewe umuhimu wa zoezi hili na kuwa tayari kuwapokea,bado wapo wengi hawajui utaratibu wa zoezi hili"Aliisitiza Balozi Kagasheki.
Mwisho.
0 Comments