Header Ads Widget

HADHA YA WANANCHI KUTEMBEA UMBALI WA KM 70 KUFUATA HUDUMA ZA AFYA YAPATA UFUMBUZI..



Na WILLIUM PAUL, SAME.


WAKAZI zaidi ya 13,000 wa Kata za Vunta na Kirangale, wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro, wanatarajia kuondokana na changamoto ya kutembea umbali wa zaidi ya kilomita 70 hadi Kituo cha Afya Hedaru na Hospitali ya Mji wa Same kufuata huduma za afya. 


Huduma hizo ni pamoja na upasuaji mkubwa na dharura, baada ya Serikali kukamilisha ujenzi wa Kituo cha Afya Vunta ifikapo Desemba 31 mwaka huu. 



Hayo yamebainishwa wakati wa ziara ya Mkuu wa Wilaya ya Same, Kasilda Mgeni akiambatana na Kamati ya Usalama ya wilaya, walipotembelea na kukagua utekelezaji wa ujenzi wa kituo hicho cha afya.



Katika maelekezo yake, Kasilda amewataka wasimamizi wa mradi kuongeza kasi ya ujenzi ili kuhakikisha unakamilika kwa muda uliopangwa na kwa viwango vinavyotakiwa ili kuwanufaisha wananchi kwa muda mrefu.



“Mradi huu ni muhimu sana kwa wananchi wa maeneo haya ya milimani, hasa Kata ya Vunta na maeneo jirani. Ongezeni kasi ya ujenzi ili wananchi waanze kunufaika, maana kwa sasa wanalazimika kutembea zaidi ya kilomita 70 na kutumia gharama kubwa za kusafiri kufuata huduma Kituo cha Afya Hedaru na Hospitali ya Same,” alisema Kasilda.


Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha kila nyaraka za mradi huo zinatunzwa ipasavyo kwani nyaraka hizo ni sehemu muhimu ya uwazi na uwajibikaji na zitasaidia Serikali kujiridhisha na thamani ya fedha zilizowekezwa. 



Vilevile amesisitiza kuwa ujenzi lazima ufuate ramani na viwango vilivyopitishwa ili mradi huo uwe na ubora na udumu kwa muda mrefu.


Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Vunta, Thomas Kalinga, ameishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kutoa fedha za kutekeleza mradi huo, akieleza kuwa utapunguza kwa kiasi kikubwa changamoto zilizokuwa zikiwakabili wananchi wa Kata ya Vunta na maeneo jirani.



Amesema mradi huo utaboresha mazingira ya utoaji huduma, kupunguza gharama na muda wa kusafiri kufuata huduma mbali na makazi yao.


Mradi wa ujenzi wa Kituo cha Afya Vunta unagharimu zaidi ya shilingi milioni 629, ambapo hadi sasa zaidi ya milioni 323 zimetumika na utekelezaji wake ulianza Februari 10, 2025 na unatarajiwa kukamilika Desemba 31, 2025.


Mwisho.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI