Header Ads Widget

DKT. MWINYI KUONGEZA THAMANI YA ZAO LA MWANI, AAHIDI BEI KUFIKIA SHILINGI 1,000 KWA KILO*


Mgombea wa Urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameahidi kuongeza thamani ya zao la mwani kwa kuhakikisha bei yake inapanda kutoka shilingi 700 hadi kufikia shilingi 1,000 kwa kilo, hatua itakayowanufaisha zaidi wakulima wa zao hilo nchini.

Akizungumza na makundi mbalimbali ya wakulima wa mwani, mpunga na wavuvi katika uwanja wa mpira wa Marumbi, Mkoa wa Kusini Unguja, Dkt. Mwinyi amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuwa bega kwa bega na wakulima hao kwa kuwa sekta hizo tatu ni nguzo muhimu katika uchumi wa buluu.

Amesema Serikali itaendelea kutoa zana za kilimo kama matrekta na mashine za uvunaji ili kuongeza tija kwa wakulima wa mpunga, sambamba na kuhakikisha pembejeo, mbolea na viwatilifu vinapatikana kwa urahisi ili kuongeza uzalishaji wa mchele wa ndani. 

Aidha, amebainisha kuwa Serikali tayari imeamua kujenga maghala ya kisasa na kuimarisha mfumo wa ununuzi wa mazao kutoka Tanzania Bara ili kudhibiti mabadiliko ya bei sokoni.

Kuhusu zao la mwani, Dkt. Mwinyi amesema Serikali itaongeza fungu la mikopo kwa wakulima, kujenga viwanda vya kusarifu mwani na kuanzisha mfumo rasmi wa ununuzi wa mwani wote utakaolimwa Zanzibar.

Amesisitiza kuwa lengo ni kuongeza thamani ya zao hilo na kuhakikisha wakulima wanapata faida kubwa kupitia uzalishaji wa mwani wenye ubora wa kimataifa.

Aidha, Dkt. Mwinyi amesema Serikali itaboresha miundombinu ya uvuvi kwa kujenga madiko, masoko ya kisasa, na kuendeleza boti kubwa za kisasa zitakazosaidia wavuvi kuongeza uzalishaji.

Ameongeza  kuwa eneo la Marumbi pia litazingatiwa katika mpango wa ujenzi wa skuli mpya kama sehemu ya kuimarisha maendeleo ya kijamii.

Dkt. Mwinyi amesisitiza kuwa mikakati yote hiyo inalenga kuongeza thamani ya uchumi wa buluu, kuimarisha kipato cha wananchi na kukuza uchumi wa Zanzibar kwa ujumla.


 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI