Header Ads Widget

BONANZA LA VETERANS NYANDA ZA JUU KUSINI KUTIKISA MBEYA.

 

Na Moses Ng’wat, Mbeya.  

Bonanza kubwa la Veterans Nyanda za Juu Kusini linatarajiwa kufanyika katika Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya kuanzia Novemba 1 hadi 2 mwaka huu.

Wachezaji wakongwe zaidi ya 2,000 kutoka mikoa sita wanatarajiwa kutumia bonanza hilo kuonesha  uzoefu, ustadi, ikiwemo  kurejesha kumbukumbu walizotambnazo enzi hizo na kutumika kama darasa kwa   kizazi kipya cha wanasoka.  


Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari Oktoba 19,2025, Katibu Mkuu wa Umoja wa Maveterans mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, Michael Ndolanga, amesema jumla ya timu 15 zinatarajia kushiriki katika Bonanza hilo, huku timu ya Rungwe Veterani ikiwa ni mwenyeji na mgeni Rasmi atakuwa Mkuu wa Wilaya hiyo, Jaffar Haniu.

Ndolanga amesema mbali na timu ya  Rungwe Veterani, Mkoa wa Mbeya pia utajumusha timu nyingine nne ambazo ni Kyela Veterans, Mbalizi Veterans, Mwanjelwa Veterans, Mbeya Legends Veterans.



Kutoka Ruvuma kutakuwepo na timu za Songea Veterans na Mbinga Veterans, wakati Mkoa wa Iringa utawakilishwa na Mkwawa Veterans, Ilula Veterans na Igowole Veterans, ambapo Mkoa wa  Njombe utashirikisha timu za Njombe Veterans na Njombe Pamoja na Mkoa wa Songwe wenyewe utawakilishwa na timu za Tunduma Veterans, Enjoy Veterans na wakiwemo mabingwa watetezi Mbozi Veterans.

Katibu Mkuu Ndolanga, ameongeza kwa kusema kuwa michuano ya Bonanza kwa wakongwe wa soko mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ilianzishwa mwaka 2019, ikiwa inafanyika mara mbili kila mwaka, na imekuwa ikitoa zawadi kwa washindi mbalimbali.

Zaidi ya ushindani wa uwanjani, bonanza hilo limekuwa chachu ya kuimarisha umoja, afya, na fursa za kiuchumi miongoni mwa wakongwe wa soka, sanjari na kusaidiana katika nyakati za misiba na matatizo ya kijamii.  

Hata hivyo, Ndolanga ametoa  wito kwa wadau wa michezo na kampuni mbalimbali kujitokeza kudhamini tukio hilo, hasa katika kugharamia zawadi, vifaa vya michezo, na jezi za timu.  

“Tunafanya haya kwa moyo wa kujitolea, lakini tungefurahia kuona wadau wanajiunga nasi ili kuongeza hamasa kwa wakongwe hawa wanaoendelea kuenzi michezo kama sehemu ya afya na umoja,” amesema Ndolanga.  

Bonanza hilo, linatarajiwa kuacha alama kubwa kwa wilaya ya Rungwe, huku wakongwe wakipata fursa ya kuonyesha bado wana miguu yenye ladha ya soka la zamani. 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI