Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Said Mtanda akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na Kongamano la kitaifa la wiki ya Ufuatiliaji, Tathimini na Kujifunza (MEL) litakalofanyika Jijini Mwanza.
Na Chausiku said
Matukio Daima Mwanza
Washiriki takribani 1000 wanatarajiwa Kushiriki kwenye Kongamano la kitaifa la wiki ya Ufuatiliaji, Tathimini na Kujifunza (MEL) litakalofanyika Jijini Mwanza kuanzia Septemba 10 hadi 13, 2025.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Said Mtanda ameeleza kuwa kongamano hilo litahusisha viongozi wa serikali, mabalozi, sekta binafsi, taasisi za elimu, vijana na wadau wa maendeleo kutoka mataifa mbalimbali.
Mkurugenzi wa Idara ya Ufuatiliaji na Tathmini ya Utendaji wa Serikali, Sakina Mwinyimkuu Akizungumza umuhimu wa kongamano hilo litakaofanyika septemba 10 mpaka 13
Amesema kuwa ufuatiliaji na tathmini ni silaha muhimu kwa serikali katika kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa wakati, kwa ubora na kwa thamani halisi ya fedha.
Mtanda ameeleza kuwa kupitia, ufuatiliaji na tathmini inayofanyika mara kwa mara imewezesha utekelezaji wa miradi yenye thamani ya Shilingi trilioni 5.6 kati ya mwaka 2021 hadi 2025.
Baadhi ya miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa Daraja la JPM-Kigongo-Busisi, reli ya kisasa ya Standard Gauge Railway (SGR), miundombinu ya vivuko, na hospitali ya kibingwa yenye hadhi ya Mkoa wilayani Ukerewe.
Lakini pia miradi mingine ni pamoja na ujenzi wa Barabara chini ya usimamizi wa TANROADS na TARURA, Soko kuu la kisasa mjini kati, mradi wa maji Butimba na Meli kubwa ya abiria na mizigo ya MV Mwanza.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Ufuatiliaji na Tathmini ya Utendaji wa Serikali, Sakina Mwinyimkuu amesema kongamano hilo litakalofanyika Mwanza ni la nne tangu kuanzishwa kwake mwaka 2022.
Mwinyimkuu amesema kongamano la kwanza lilifanyika Dodoma mwaka 2022, la pili Arusha mwaka 2023 na la tatu lilifanyika Zanzibar mwaka 2024, ambapo kila mwaka limekuwa likileta matokeo chanya kwa taifa kutokana na maazimio ya kwanza ya kongamano yalihusu kuimarisha miundo na mifumo ya serikali katika kusimamia utendaji wa Serikali.
"Kwa ujumla baada ya maazimio hayo utekelezaji ulianza ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alitoa kibali kwa wizara zote kuwa na vitengo vya ufuatiliaji na tathmini ili kufuatilia kwa ukaribu utekelezaji wa afua mbalimbali za Serikali ambapo hadi sasa mikoa yote tayari imeanzisha vitengo vya MNE pamoja na mamlaka za Serikali za mitaa hatua hiyo imetajwa kuwa miongoni mwa mafanikio makubwa ya maazimio ya makongamano yaliyopita." amesema Mwinyimkuu
Aidha, amesema tathmini zilizopita zinaonesha mwamko mkubwa katika eneo la ufuatiliaji na tathmini ambapo miradi yote inafanyiwa tathmini na kupitia kongamano hili miradi mingi itaenda kuleta tija kwa wananchi.
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, James Kilabuko amemshukuru Mkuu wa mkoa kwa kukubali kuwa mwenyeji wa kongamano hilo huku akiongeza kuwa maandalizi ya shughuli hiyo yanaendelea vizuri.
kongamano hilo lenye kauli mbiu isemayo "kuimalisha Ufuatiliaji na Tathmini katika Ngazi ya Jamii ili kuleta maendeleo endelevu" linatarajia kushirikisha Nchi 18, huku Mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa.
0 Comments