Na Hamida Ramadhani, Matukio Daima Dodoma
KATIKA harakati za kupunguza madhara ya kiafya na kimazingira yanayosababishwa na matumizi ya kuni na mkaa, wananchi wametakiwa kuachana na nishati hizo na kuhamia kwenye matumizi ya majiko yanayotumia umeme na sola kupitia kampeni ya kitaifa ya Pika Smart.
Ikiwa ni kampeni ya mkoa wa tano kwa Dodoma huku lengo likiwa ni kuelimisha jamii kuhusu faida za kutumia nishati safi kwa gharama nafuu, huku ikilenga kupunguza utegemezi wa nishati zisizo salama na zisizo endelevu.
Akizungumza wakati wa kampeni hiyo Sememba Mosi jijini Rightness Felix Balozi wa Pika Smart, amesema kuwa matumizi ya kuni na mkaa yana gharama kubwa kwa familia na yana madhara kwa afya na mazingira.
“Kwa kutumia majiko ya umeme, mtu anaweza kupika kwa gharama ndogo sana. Kwa mfano, unaweza kutumia shilingi 1,000 tu na ukapika mlo wako bila moshi wala madhara ya kiafya tuna vifaa salama kabisa, tofauti na mitazamo iliyokuwepo awali kuwa majiko ya umeme yanapiga shoti,” amesema Felix.
Amewahimiza wananchi kuchukua muda wa kuelewa matumizi ya majiko hayo, akisema kuwa elimu ni muhimu kwa matumizi sahihi na salama ya vifaa hivyo.
Kwa mujibu wa Felix amesema ,kampeni ya Pika Smart inalenga kuhakikisha kuwa kufikia mwaka 2030, Watanzania wengi wanatumia nishati safi majumbani mwao.
"Tayari baadhi ya wananchi wameanza kutumia majiko ya sola, ambayo ni mbadala mzuri kwa maeneo yenye changamoto ya umeme wa gridi," Amesema .
Nakuongeza kusema "Kwa sasa, kampeni hiyo imefika katika mikoa mitano nchini, ikiwemo Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Mbeya na Dodoma, ambapo wananchi wameonesha mwitikio mzuri lakini bado changamoto ya gharama imekuwa kikwazo kwa wengi,".
Eliudi Swai, Meneja wa Positive Cooker Blanch Kanda ya Kati, amesema kuwa majiko hayo yameundwa kwa lengo la kupunguza muda wa kupika na gharama zinazowakabili kina mama wa Kitanzania.
“Majiko haya yanarahisisha maisha kwa kina mama kwa kuwa yanapika haraka, hayatoi moshi, na hayahitaji kuni wala mkaa ni mageuzi katika sekta ya nishati ya nyumbani,” amesema Swai.
Hata hivyo, baadhi ya wananchi katika kampeni hiyo walieleza kuwa bei ya majiko hayo bado ni juu, kwani yanauzwa kwa wastani wa shilingi 100,000, kiasi ambacho Mtanzania wa kawaida hawezi kumudu kirahisi.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi, Selina Kaizari aliomba majiko hayo yatolewe kwa mfumo wa mkopo ili kuwawezesha watu wa kipato cha chini kunufaika nayo.
“Tunaomba kama kuna uwezekano wa kupata majiko haya kwa mkopo yana faida nyingi lakini si kila mmoja anaweza kumudu gharama mara moja,” amesema Kaizari.
Kampeni ya Pika Smart ni sehemu ya mkakati wa kitaifa wa kuhakikisha jamii inapunguza utegemezi wa nishati chafu na kuchangia katika juhudi za kulinda mazingira, afya za wananchi na kupambana na mabadiliko ya tabianchi.
Mwisho
0 Comments