Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amewataka waajiri wa taasisi za umma kuhakikisha wanalipa stahiki za madereva kwa wakati, kutoa mafunzo ya mara kwa mara, kutekeleza ipasavyo miundo ya ajira na kuwapa motisha ili kuongeza tija katika utendaji kazi wao.
Akizungumza jijini Dodoma wakati wa kufungua Mkutano Mkuu wa Chama cha Madereva wa Serikali Tanzania (CMST), Waziri Mkuu amesema madereva wa Serikali wana mchango mkubwa katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku ya Serikali na hivyo wanapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa.
"Waajiri mnapaswa kuhakikisha madereva wanalipwa stahiki zao kwa wakati, wanapewa mafunzo stahiki na kuzingatiwa katika motisha mbalimbali. Hii itawajengea morali na kuongeza ufanisi katika kazi zao," amesema Majaliwa.
Aidha, amesisitiza kuwa madereva wanawajibu wa kufanya kazi kwa weledi na nidhamu ya hali ya juu, ikiwa ni pamoja na kuhakiki usalama wa vyombo vya usafiri, abiria, mizigo na nyaraka za Serikali.
“Madereva mnatakiwa kufanya ukaguzi wa gari kabla na baada ya safari, kujaza na kutunza taarifa za safari na matengenezo kwa uaminifu mkubwa, pamoja na kutumia vifaa vya kisasa vya usalama,” ameongeza.
Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega aamesema madereva ni mhimili muhimu wa shughuli za Serikali, hivyo nidhamu na uadilifu vinapaswa kuwa dira ya kada hiyo.
Naye Katibu Mkuu wa CMST, Castro Nyabange alimpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha maslahi ya watumishi wa umma wakiwemo madereva, hususan kupitia upandishaji wa mishahara.
Mkutano huo uliobeba kaulimbiu “Dereva wa Serikali, Epuka Ajali, Linda Gari Lako na Watumiaji Wengine wa Barabara na Oktoba Shiriki Uchaguzi Mkuu” ulihudhuriwa na zaidi ya madereva 2,500 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.
0 Comments