Na Fadhili Abdallah,Kigoma
Mgombea ubunge jimbo la Kasulu mjini kwa tiketi ya CCM Profesa Joyce Ndalichako amesema kuwa utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya wananchi uliofanywa na serikali ya awamu ya sita ya Rais Samia Suluhu Hassan unafanya wagombea wa Chama Cha mapinduzi kuwa washindi hata kabla kura hazijapigwa.
Profesa Ndalichako ambaye amesimamishwa na CCM kugombea kwa awamu ya pili ubunge katika jimbo hilo alisema hayo akizindua kampeni za uchaguzi uzinduzi uliofanyika kijiji cha Ruhita wilaya ya Kasulu ambapo alisema kuwa miaka mitano aliyokuwa mbunge katika jimbo la Kasulu mjini kazi kubwa imefanyika ambayo imeiweka serikali ya CCM kwenye mioyo ya watanzania.
Mgombea ubunge wa jimbo la Kasulu Mjini kwa tiketi ya CCM Profesa Joyce Ndalichako akizungumza katika mkutano wa kampeni kwenye kijiji cha Ruhita wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma
Alisema kuwa kabla mwaka 2020 jimbo hilo lilikuwa na changamoto kubwa ya miundo mbinu ya barabara lakini kazi iliyofanyika kwa sasa imelifanya sehemu kubwa ya barabara za jimbo hilo kupitika ikiwemo sehemu kubwa ya barabara za lami huku shule mpya tisa za sekondari zikijengwa na shule sita mpya za msingi.
Akieleza kuhusu miradi ya maji alisema kuwa ipo miradi mbalimbali midogo ilitekelezwa na kupunguza changamoto ya maji kwa wananchi wa jimbo hilo ambapo kwa sasa serikali inamalizia mradi mkubwa wa maji wenye thamani ya shilingi Bilioni 35 ambao utaondoa kabisa changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi wa jimbo hilo.
Sehemu ya wananchi wa jimbo la Kasulu mjini waliojitokeza kwenye uzinduzi wa kampeni za uchaguzi mkuu katika jimbo hilo uliofanyika kijiji cha Ruhita wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma
Akizungumza katika uzinduzi huo wa kampeni Katibu wa CCM mkoa Kigoma, Christopher Pallangyo amewataka wagombea wa nafasi za ubunge na udiwani mkoani humo kutumia ilani ya uchaguzi ya CCM kwani imesheheni mambo makubwa ambayo chama hicho kimeelekeza kufanywa na serikali mambo ambayo yanagusa maisha ya wananchi moja kwa moja.
Katibu wa CCM mkoa Kigoma Christopher Pallangyo (kulia) akimtambulisha Mgombea ubunge wa jimbo la Kasulu Mjini kwa tiketi ya CCM Profesa Joyce Ndalichako kwa wapiga kura wa jimbo hilo katika mkutano wa kampeni kwenye kijiji cha Ruhita wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma
Pallangyo alisema kuwa haina maana kutumia nguvu kujibu mambo ya hovyo yanayozungumzwa na wapinzani kwani mambo yaliyofanyika vipindi vilivyopita katika utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM yanapaswa kuwa ajenda kubwa ya wagombea wakieleza yaliyofanywa na serikali hivyo wagombea wanapaswa kujivunia ilani hiyo.
0 Comments