Header Ads Widget

UJIO WA MV MWANZA KUCHOCHEA UCHUMI WA KANDA YA ZIWA.

 

Na Shemsa Mussa -Matukio Daima Media.

Kagera.

Meli mpya ya MV Mwanza iliyosubiriwa kwa muda mrefu hatimaye imekamilika kwa asilimia 99, baada ya ujenzi wake kuchukua takribani miaka mitano. Ujenzi huo ulianza kipindi cha uongozi wa Hayati John Pombe Magufuli akiwa ameacha mradi huo ukiwa umekamilika kwa asilimia 30.

Meli hiyo ambayo imegharimu zaidi ya shilingi bilioni 126 ina uwezo wa kubeba abiria 1,200 na mizigo yenye uzito wa tani 400. Aidha, itachukua muda wa kati ya saa 6 hadi 6 na nusu kusafiri katika Ziwa Victoria.

Akizungumza kuhusu mradi huo, mwakilishi wa mkandarasi kutoka kampuni ya Gas Entec Co. Ltd, Eng. Rayton Kwembe, alisema meli hiyo ni ya kisasa na itarahisisha usafiri na biashara katika ukanda huo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Huduma za Meli Tanzania (TASHICO), Ndg. Eric Hamiss, alitoa shukrani kwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha meli hiyo inakamilika. Alibainisha kuwa ujio wa MV Mwanza utakuwa chachu ya ukuaji wa uchumi si tu kwa Tanzania bali pia kwa nchi jirani, kwani meli hiyo itapita hadi Port Bell nchini Uganda ikiwa na abiria na mizigo.

Naye Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Kagera, Karim Amri, alisema kukamilika kwa meli hiyo ni uthibitisho wa utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi, na akaishukuru serikali kwa juhudi hizo.

Baadhi ya wananchi akiwemo Anastazia Kweyamba na Amza Mzee, waliipongeza serikali kwa kukamilisha meli hiyo, wakibainisha kuwa itaondoa changamoto za usafiri na kurahisisha shughuli za biashara katika Kanda ya Ziwa.

MWISHO.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI