Header Ads Widget

DKT. MWINYI AAHIDI SOKO KUBWA LA KISASA KINYASINI, ASEMA HATUNA SABABU YA KUSHINDWA

 

Mgombea wa Urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameahidi kujenga soko kubwa la kisasa katika eneo la Kinyasini, Mkoa wa Kaskazini Unguja, mara baada ya kushinda uchaguzi mkuu. 

Dkt. Mwinyi amesema soko hilo litakuwa chachu ya kuinua biashara za wakulima, wafanyabiashara wadogo na wajasiriamali, huku likiwa na miundombinu ya kisasa inayokidhi mahitaji ya wakati huu.

Akizungumza na wafanyabiashara wa soko la Kinyasini, Dkt. Mwinyi amewahakikishia mazingira bora ya kufanyia biashara, upatikanaji wa mikopo isiyo na riba pamoja na elimu ya biashara ili kuongeza ufanisi na maendeleo ya sekta ya biashara Zanzibar.

Amesema serikali yake imepanga kuendelea na mpango wa ujenzi wa maeneo ya biashara kuanzia mwaka 2025 hadi 2030, ambapo soko la Kinyasini limepewa kipaumbele kutokana na kuzidiwa na wingi wa wafanyabiashara.


Aidha, ameahidi kuwa soko hilo litakuwa na eneo la kutosha kwa ajili ya maegesho ya magari ili kutatua changamoto ya msongamano na usumbufu kwa wateja. 

Amesema tayari serikali imetenga shilingi bilioni 96 kwa kuwawezesha Wafanyabiashara na fedha hizo zitaongezwa mara mbili ya Uwekezaji uliopo sasa.

 Dkt. Mwinyi amewaomba wafanyabiashara na wananchi wa Kinyasini kumpa ushirikiano ili kuendeleza utekelezaji wa ahadi hizo, akisisitiza kuwa kila alichokiahidi katika miaka iliyopita kimefanikiwa kutekelezwa. 

“Hatuna sababu ya kushindwa kujenga soko la Kinyasini. Ushirikiano wenu ndio utakuwa nguvu yetu,” amesema.

MWISHO.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI