Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma
MAMLAKA ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi (TASEZA) imetenga jumla ya hekta 607 katika eneo la Nala, jijini Dodoma, kwa ajili ya maendeleo ya viwanda na uwekezaji wa huduma mbalimqali, ikiwa ni sehemu ya mpango mkakati wa serikali wa kukuza sekta ya viwanda nchini.
Akizungumza wakati wa ziara ya eneo hilo la uwekezaji na kukagua maendeleo ya ujenzi wa kiwanda cha kusindika mafuta ya kupikia cha Karibu Natural Limited, Meneja wa Kanda ya Kati wa TASEZA, Venance, amesema eneo hilo limekusudiwa kuvutia wawekezaji wa ndani na nje katika sekta mbalimbali ikiwemo uzalishaji wa mafuta ya kupikia, madawa, teknolojia, vifaa vya matumizi ya nyumbani, pamoja na uchakataji wa madini.
“Kiwanda hiki ni mojawapo ya miradi iliyosajiliwa kupitia kituo chetu Mradi huu una thamani ya zaidi ya dola milioni 4 na unatarajiwa kutoa ajira kwa wafanyakazi zaidi ya 100. Tayari uko katika hatua za mwisho za ujenzi na utakapoanza kazi utakuwa na mchango mkubwa kwa uchumi wa mkoa huu na taifa kwa ujumla,” alisema.
Aidha, Venance Mashiba amesema kuwa serikali imeweka mazingira rafiki ya uwekezaji katika maeneo maalum, ambapo wawekezaji watakaowekeza kuanzia dola milioni 5 watapatiwa ardhi bure pamoja na motisha mbalimbali za kikodi, ikiwa ni pamoja na punguzo la ushuru wa kuingiza malighafi kutoka nje ya nchi.
Tangu kuzinduliwa kwa kampeni ya kuhamasisha uwekezaji katika eneo hilo tarehe 12 Agosti mwaka huu, tayari wawekezaji wanne wa ndani wamewasilisha maombi yao rasmi, huku mazungumzo yakiendelea kati ya TASEZA na wawekezaji wa kimataifa wanaotarajiwa kuingia ubia na Watanzania.
Kwa upande wake, Meneja Uhusiano na Mawasiliano wa TASEZA, Pendo Gondwe, amesema kuwa lengo la ziara hiyo ni kuwaonesha wadau maandalizi yaliyopo na kuwahamasisha kutumia fursa ya uwekezaji katika eneo la Nala, ambalo tayari linafikika kwa urahisi na lina miundombinu ya msingi.
“Tunataka jamii na wawekezaji wajue kuwa maeneo ya uwekezaji yapo tayari. Tumekuja kushuhudia mapinduzi ya kweli ya ujenzi wa viwanda nchini. Tunatarajia hadi kufikia Desemba mwaka huu, tuwe tumepokea angalau viwanda 100 katika maeneo ya kiuchumi, ikiwemo hapa Nala,” amesema Bi. Gondwe.
Mkurugenzi wa Karibu Natural Limited, Bw. Varum Giyal, amesema wameamua kuwekeza nchini Tanzania kutokana na mazingira ya utulivu, sera nzuri za kiuchumi, pamoja na dhamira ya dhati ya serikali katika kukuza uwekezaji wa ndani na nje.
“Tanzania ni mahali sahihi pa kuwekeza. Tumepokelewa vizuri na tumeona nia ya kweli ya kusaidia wawekezaji. Tunatarajia kutoa ajira nyingi na kushiriki katika ukuaji wa uchumi wa taifa,” alisema Giyal.
TASEZA imesisitiza kuwa matarajio ya muda mrefu ni kuhakikisha kuwa eneo la Nala linakuwa kitovu cha viwanda katika Kanda ya Kati na linachangia kwa kiasi kikubwa katika kufanikisha azma ya Tanzania ya kuwa nchi ya viwanda ifikapo mwaka 2030.
Mwisho
0 Comments