Header Ads Widget

SUA WAOKOA MTOTO WA TEMBO KILOMBERO

 


Na Farida Mangube, Kilombero, Morogoro 

Timu ya wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) ikiongozwa na Dr. Richard Samson, imefanikiwa kuokoa mtoto wa tembo aliyenaswa na mtego kando ya Mto Ruhidgi, katika Pori la Akiba la Kilombero, Wilaya ya Malinyi, Morogoro. 

Mtego huo, uliotengenezwa kwa kamba ngumu, ulikuwa umemnasa mguu wa mbele wa mtoto huyo wa tembo kwa siku mbili, na hivyo kuhatarisha maisha yake kwa sababu hakuweza kutembea, kutafuta chakula au maji.

Uokoaji huu ulifanywa mnamo 19 Septemba 2025, kwa ushirikiano na Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania (TAWA), ambayo inasimamia Pori la Akiba la Kilombero. Wataalamu waliweza kuondoa kamba na kuhakikisha mtoto wa tembo anarudi katika afya njema, kisha kuungana na familia yake ya asili huku akiendelea kupewa uangalizi wa karibu.



Aidha  tukio hili linakidhi wajibu wa Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori Na. 5 ya 2009, inayokataza ujangili, kujeruhi au kuua wanyamapori katika hifadhi. Pia linahimiza utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Wanyamapori ya 2007, inayohimiza ushirikiano kati ya serikali, taasisi za elimu na jamii katika kuimarisha uhifadhi.


Dr. Richard Samson kutoka SUA amesema, “Uokoaji huu ni mfano wa jinsi elimu, ujuzi wa kitaaluma na ushirikiano kati ya taasisi za serikali na za elimu ya juu unavyoweza kuokoa maisha ya wanyamapori na kudumisha maliasili yetu.” Huku akisisitiza SUA kudumisha mashirikiano na taasisi za uhifadhi 


Kwa upande wa TAWA imeahidi kuendelea kumlinda mtoto wa tembo huyu na kuhakikisha anaendelea kuimarika katika familia yake ya porini. 


Tukio hili linaendana na mkataba wa CITES (1973) unaolinda wanyamapori walioko hatarini kutoweka. Pia linachangia katika utekelezaji wa SDG 15 (kulinda mifumo ya ikolojia ya nchi kavu), SDG 13 (kupambana na mabadiliko ya tabianchi kupitia uhifadhi wa ikolojia), na SDG 17 (kuimarisha ushirikiano kati ya serikali, jamii na taasisi za elimu).



Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI