Header Ads Widget

*SERIKALI YAFIKISHA MAWASILIANO MSOLOKELO, MVOMERO – MOROGORO*


Wakazi wa kijiji cha Msolokelo, Kata ya Pemba wilayani Mvomero mkoani Morogoro, sasa wanafurahia huduma bora za mawasiliano baada ya kukamilika kwa ujenzi wa mnara uliojengwa na kampuni ya simu ya Vodacom kwa ruzuku inayotolewa na Serikali  kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF)

Akizungumza na wananchi wa kijiji hicho mara baada ya kukagua maendeleo ya mnara huo, ukiwa ni miongoni mwa minara 758 inayoendelea kujengwa nchini kote, mradi ambao utekelezaji wake umefikia asilimia 97, Mtendaji Mkuu wa UCSAF Mhandisi Peter Mwasalyanda amesema, Serikali imedhamiria kuhakikisha kuwa kila Mtanzania anafikiwa na huduma za mawasiliano bila kujali mahali anapoishi. 

Kwa muda mrefu, wananchi wa Msolokelo wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya ukosefu wa huduma za mawasiliano, hali iliyowalazimu kupanda milimani na hata kwenye miti ili kupata mtandao wa simu kwa mawasiliano ya dharura na shughuli za kila siku. 


Kukamilika kwa ujenzi wa mnara huu sasa, kumewaletea suluhu ya kudumu na kukiweka kijiji hicho kwenye ramani mpya ya mawasiliano ya kisasa, kwa kuwa mnara huo umejengwa katika kiwango cha teknolojia ya 2G,3G na 4G.

Ujenzi wa mnara huo ni matokeo ya ziara ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Jerry Silaa, alipokagua hali ya mawasiliano katika Kata ya Pemba, ambapo alifika katika kijiji cha Msolokelo mwezi Disemba 2024 na kuiagiza UCSAF kushughulikia changamoto ya mawasiliano iliyokuwa inawakabili wananchi wa kijiji hicho.

Kukamilika kwa ujenzi wa mnara huu kunadhihirisha wazi dhamira ya Serikali ya awamu ya Sita chini ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuhakikisha wananchi wote, mijini na vijijini, wananufaika kwa usawa na maendeleo ya TEHAMA nchini, hatua muhimu kuelekea Tanzania yenye uchumi wa kidigitali.





Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI