Header Ads Widget

NCT NA SBL YAZINDUA PROGRAMU YA MAFUNZO YA WATOA HUDUMA YA VINYWAJI JIJINI ARUSHA

Na,Jusline Marco;Arusha

Kampuni ya Bia ya Serengeti kwa kushirikiana na Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT) wamezindua rasmi awamu ya pili ya programu ya ‘Learning for Life’ katika Tawi la NCT Arusha wakitanua ushirikiano ulioanzishwa jijini Dar es Salaam tangu Septemba 2024.


Akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa programu hiyo uliyofanyika katika Chuo cha Taifa cha Utalii Kampasi ya Arusha Mkuu wa chuo hicho Dkt.Florian Mtey amesema sekta ya utalii ni nguzo muhimu katika uchumi wa taifa kwa kuchangia asilimia 17 ya pato la Taifa na asilimia 25 ya Mapato ya fedha za kigeni sambamba na kuajiri watu takribani Milioni 1.4 kwa mwaka kupitia njia za Moja kwa Moja na zisizo za Moja kwa Moja.


Dkt. Mtey amesema mafunzo hayo ni nyenzo muhimu ya kufanikisha lengo la serikali la kufikia watalii Milioni 5 na mapato ya dola za marekani billioni 6 ifikapo mwaka 2030 kwa Kuimarisha ubora wa huduma zinazotolewa ambapo amesema uzinduzi huo ni muendelezo wa safari iliyoanzia jijini Dar es salaam mwaka Jana chini ya ushirikiano wa Chuo hicho na kampuni ya SBL .


Ameongeza kuwa matokeo ya programu hiyo yamedhihirisha wanafunzi takribani 100 waliohitimu Mei 2025 kuongeza ujuzi, kujiamini na uwezo wa kuingia sokoni huku asilimia 45 ya wanafunzi hao wamepata ajira na mafunzo kwa vitendo ambapo amesema hatua hiyo ni uthibitisho kuwa mafunzo hayo yanalingana na mahitaji ya waajiri na kuweza kubadilisha maisha ya vijana na kuinua viwango vya huduma katika sekta ya Utalii.


Ameeleza kuwa kutoka na mafanikio ya awamu ya kwanza,awamu hiyo ya pili kufanyika jijini Arusha imeongeza mahitaji ya wataalamu katika sekta ya ukarimu huku alisema wanafunzi 150 wanatarajiwa kupata njia ya moja kwa moja kuelekea fursa za ajira katika hoyeli, malazi ya watalii, migahawa na waendeshaji wa Utalii wa eneo lenye kasi ya ukuaji.


Amesisitiza kuwa programu hiyo ni mchanganyiko wa mafunzo ya nadharia na vitendo yaliyoimarishwa na uendeshaji wa baa,ubunifu wa vinywaji na huduma kwa wateja sambamba na kuwajengea uwezo wa mawasiliano, uongozi pamoja na kuwapa stadi za kifedha na stadi za maisha ambazo zitawasaidia Kila mahali watakapokwenda

Amebainisha kuwa mafunzo hayo yanaonyesha thamabi ya ubia wa sekta binafsi na za Umma ambapo ushirikiano wa NCT na SBL hauishii kwa utoaji wa mafunzo tu Bali unaongeza ujuzi wa vijana, kuboresha huduma katika maeneo ya starehe na mapokezi sambamba na kuwa wageni uzoefu bora  hivyo Kuimarisha Utalii kama injini ya uchumi wa Taifa na kuongeza ajira.


Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mauzo wa Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) Bw.Christopher Gitau amesema kuwa wao kama SBL wanaamini kwamba kuwekeza kwa vijana ni kuwekeza kwenye mustakabali wa jamii nzima ambapo kupitia mafunzo hayo wanawapa vijana stadi za kiufundi na kuwajengea uwezo wa kuwa viongozi, wajasiriamali na wachangiaji wakuu wa ukuaji wa sekta ya ukarimu na utalii nchini.


Ameeleza kuwa programu ya ‘Learning for Life’ ni sehemu ya ajenda endelevu ya SBL, ikidhihirisha dhamira yake ya muda mrefu ya kuwekeza kwa jamii, kujenga uwezo na kuwawezesha vijana wa Kitanzania ambapo kupitia programu hiyo watatoa njia mpya za ajira na kuimarisha zaidi sekta ya utalii na ukarimu nchini Tanzania.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI