Na Hadija Omary
LINDI....Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge anayemaliza muda wake wa Jimbo la Ruangwa, Kassim Majaliwa, amewahaga rasmi wakazi wa jimbo hilo na kumtakia heri mrithi wake wa kisiasa, Kasper Mmuya, katika safari yake ya kuwania ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Majaliwa alitoa ujumbe huo wakati wa uzinduzi rasmi wa kampeni za Chama cha mapinduzi (CCM) ngazi ya mkoa, zilizofanyika katika viwanja vya Likangala, Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi. Mkutano huo mkubwa ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama na serikali, huku Majaliwa akiwa mgeni rasmi.
Katika hotuba yake, Majaliwa aliwataka wananchi wa Ruangwa kumpa ushirikiano wa kutosha Kasper Mmuya, ambaye ndiye mgombea ubunge wa CCM katika jimbo hilo. Aliahidi kuendelea kuwa bega kwa bega na mgombea huyo katika safari ya kuliongoza jimbo hilo, akieleza kuwa yuko tayari kusaidia kwa hali na mali.
Majaliwa pia alitumia jukwaa hilo kuwanadi wagombea wa ubunge na udiwani wa CCM kwa majimbo na kata zote za mkoa wa Lindi, sambamba na kuwakabidhi rasmi ilani ya chama hicho. Alieleza mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita, akisisitiza umuhimu wa kuyaendeleza kupitia viongozi wanaoamini katika dira ya chama.
Kwa upande wake, Kasper Mmuya aliwaeleza wananchi kuwa hana mpango wa kuanzisha miradi mipya bali atatekeleza na kumalizia ile iliyoanzishwa na mtangulizi wake, Kassim Majaliwa. Alisema nia yake ni kuona maendeleo yanayoendelea bila kupoteza mwelekeo uliokuwepo
Wananchi wa Ruangwa wameonesha imani kubwa kwa Mmuya, wakieleza kuwa ana uwezo na uzoefu wa kutosha kuendeleza maendeleo ya jimbo hilo. Aidha, walitumia fursa hiyo kumkabidhi changamoto mbalimbali, ikiwemo umaliziaji wa ujenzi wa barabara ya Nanganga–Ruangwa na utatuzi wa migogoro kati ya wakulima na wafugaji.
Tukio hilo limeacha alama ya kihistoria kwa wakazi wa Ruangwa, ambao walijitokeza kwa wingi kuonyesha mshikamano wao na matumaini kwa mustakabali wa jimbo hilo kupitia mgombea mpya wa CCM.









0 Comments