
Na Fadhili Abdallah, Kigoma
IMEELEZWA kuwa ujenzi wa mabweni katika shule za sekondari nchini umekuwa na mchango mkubwa katika kuongeza ufaulu wa wanafunzi ambapo imefanya idadi kubwa ya wanafunzi wanaosoma shule za bweni kufaulu kwa alama za juu jambo linalowapa nafasi nzuri ya kuendelea na masomo ya juu ikiwemo vyuo vikuu.
KIONGOZI wa mbio za mwenge wa uhuru, Ismail Alli Ussi amesema hayo akizindua bweni la wanafunzi wa kidato cha tano na sita katika shule ya Sekondari ya Buronge manispaa ya Kigoma Ujiji ambapo alisema kuwa kwa sasa kumekuwa na idadi kubwa ya wanafunzi wanaofaulu na kwenda vyuo vikuu ndani na nje ya nchi.
Ussi alisema kuwa Rais Samia amedhamiria kuiondoa Tanzania kuwa nchi ya wajinga wasiojua kusoma na kuandika na kuifanya kuwa nchi ya wasomi wenye wataalam kila fani hivyo ujenzi wa mabweni katika shule za sekondari umekuwa kichocheo katika utekelezaji wa mipango hiyo.
Kiongozi huyo wa mbio za Mwenge alisema kuwa Mwenge wa uhuru umeshuhudia ujenzi wa mabweni ya wanafunzi katika maeneo mbalimbali nchini ikiwa ni moja ya mikakato ya uboreshaji wa sekta ya elimu ili kutoa nafasi ya kujifunza na kufundishia kwa kuondoa usumbufu wa wanafunzi kutembea umbali mrefu kufuata masomo na kuongeza ufaulu.
Awali akisoma taarifa ya mradi huo Mhandisi wa ujenzi wa manispaa ya Kigoma Ujiji, Julius Samwel alisema kuwa kiasi cha shilingi milioni 165.2 zimetumika kwa ajiili ya utekeleaji wa mradi huo ambao kiasi cha shilingi milioni 136 zimetolewa kupitia mradi wa lipa kwa matokeo (EP4R) na shilingi milioni 29 zimetolewa na Halmashauri kutoka mapato ya ndani na mradi umefikia asilimia 91 utaanza kuchukua wanafunzi Julai 2026.
Akisoma taarifa ya mwenge wa uhuru kwa kiongozi wa mwenge ulipoingia katika manispaa hiyo Mkuu wa wilaya Kigoma,Dk.Rashid Chuachua alisema kuwa ukiwa katika manispaa hiyo Mwenge huo wa uhuru utatembelea miradi saba yenye thamani ya shilingi Bilion i 48.6 ikiwemo miradi ya elimu, afya, barabara, utawala bora na miradi ya maji.
Mwisho.


0 Comments