Header Ads Widget

KISINIA RESTAURANT YAWAKUMBUKA WATOTO YATIMA WA CHAUWAMA, YAFANYA MATENDO YA HURUMA


Na mwandishi wetu

Kampuni ya Kisinia Restaurant imeandaa dhifa ya chakula cha pamoja kwa watoto yatima katika kituo cha CHAUWAMA (Chama cha Kuwalea Watoto Waishio kwenye Mazingira Magumu) kilichopo Sinza Mori, Dar es Salaam mapema September 1, 2025.

Mlezi wa kituo hicho, Bi. Neema Jerald, amesema kituo kinatunza watoto 64 wenye umri kuanzia miaka 2 hadi 18. Baadhi wana mzazi mmoja, wengine hawana kabisa, huku wengine wakiwa na changamoto za ulemavu na afya ya akili.

Neema Jerald, mlezi wa watoto CHAUWAMA akiishukuru Kisinia Restaurant kwa kuwapatia msaada

“Majukumu yetu ni kuhakikisha watoto wanapata afya njema, elimu kuanzia chekechea hadi chuo, pamoja na makazi salama. Tumeshuhudia watoto wakikua na kuondoka wakiwa na uwezo wa kujitegemea,” alisema Neema.


Hata hivyo, alieleza changamoto kubwa zinazowakabili ni utofauti wa mahitaji ya makundi ya watoto, pamoja na uharibifu wa jengo moja baada ya kuungua moto.

“Tunaomba msaada wa chakula, umeme, maji safi na malazi. Pia tunahitaji msaada katika upanuzi wa majengo mapya,” aliongeza.

Kwa upande wao, Kisinia Restaurant kupitia mchekeshaji Sabato Peter, wamesema dhifa hiyo ni sehemu ya kugusa maisha ya watoto hao na kuwapa tumaini.

Sabato Peter, mchekeshaji na msemaji kutoka Kisinia Restaurant akitoa wito kwa wadau wenye uwezo kuunga mkono kusaidia watoto yatima 


“Tumeleta sabuni, taulo za kike, vifaa vya shule, vyakula, na vifaa vya usafi. Zaidi ya yote, tumewapa faraja kwamba wanapendwa,” alisema Sabato.

Naye Hadija Ahmad kutoka Kisinia Restaurant aliongeza.

Hadija Ahmad kutoka kampuni ya Kisinia Restaurant akiishukuru CHAUWAMA kuwapokea

“Tumekuja kuwatia moyo watoto hawa. Tunamwomba Mwenyezi Mungu atubariki zaidi ili tuendelee kukumbuka watoto wetu. Huu ni mwito kwa wengine pia kuguswa na kushiriki kutoa msaada.”

Kituo cha CHAUWAMA kilianzishwa mwaka 1998 na Bi. Sauda, na kwa sasa kinasimamiwa na Ndugu Hassan Hamis.








Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI