Header Ads Widget

KIBAHA YATOA HATI ZA UMILIKI ARDHI PANGANI.


Na Mwandishi Wetu, Matukio Daima Media Kibaha

MANISPAA ya Kibaha imetoa hati za umiliki wa ardhi kwa wananchi 180 kwenye Kata ya Pangani Wilayani Kibaha ikiwa ni mpango wa Serikali wa kuhakikisha kila eneo la ardhi linapimwa.

Akikabidhi hati hizo kwenye Kata ya Pangani Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson John amesema kuwa upatikanaji wa hati hizo ni mkombozi kwa wananchi kumiliki maeneo yao kisheria.

John amesema kuwa umiliki huo wa kisheria utaondoa migogoro ya ardhi ambayo katika eneo hilo ilikuwa mingi na kusababisha changamoto kubwa.

"Hadi sasa hati 7,000 zimeandaliwa huku viwanja 18,000 tayari vimepimwa na ramani 8,000 zitatolewa kwa wananchi hivyo kilichobaki ni wananchi kulipia ili wapewe hati zao,"amesema John.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha Dk Rogers Shemwelekwa amesema kuwa kufuatia viwanja hivyo kupimwa wananchi wasiuze kwa hatua kama ni kuuza wauze kiwanja chote kwani mtu akiuziwa hatua hatoweza kupa hati ya umiliki.

Shemwelekwa amesema kuwa katka kurahisisha upatikanaji wa hati taratibu zitafanywa kwenye Kata kwa kufanya malipo na ramani zitapatikana hapo ili kuwaondolea usumbufu wa kwenda ofisi za Manispaa.

Amesema kuwa wasikubali kupotoshwa kwani wameteseka muda mrefu kama kuna changamoto wawatumie viongozi wao na kuachana na matapeli wa ardhi.

Naye Msajili wa Hati Msaidizi Mkoa wa Pwani Burton Rutta amesema kuwa gharama za maombi zimeshuka kutoka 20,000 hadi 5,000 hivyo hata mwananchi wa hali ya chini ana uwezo wa kupata hati ya umiliki wa ardhi.

Rutta amesema kuwa faida ya kumiliki ardhi kisheria na kupata hati mbali ya kupunguza migogoro ya ardhi pia inasaidia kukopa benki na hata kuweka dhamana mahakamani na kwenye maeneo ya uwekezaji fidia hupatikana haraka.

Mkazi wa Kidimu Mwanaid Mangu amesema kuwa anaishukuru serikali kwa kuwapatia hati hizo kwani zitawasaidia kuwa na uhalali wa umiliki na kuondoa utapeli wa ardhi.

Mangu amesema kwa sasa wataishi kwa amani sababu watu walikuwa wakiwatapeli watu viwanja vyao na kuviuza mara mbili mbili na kusababisha migogoro.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI