Burkina Faso inasema imeanzisha mfumo wa viza bila malipo kwa raia wa Afrika, kwa nia ya kuwezesha usafirishaji wa watu na bidhaa ndani ya nchi.
Uamuzi huo ulichukuliwa Alhamisi, wakati wa mkutano wa baraza la mawaziri ulioongozwa na kiongozi wa kijeshi Kapteni Ibrahim Traoré
"Kuanzia sasa, raia yeyote kutoka nchi ya Kiafrika anayetaka kwenda Burkina Faso hatalipa kiasi chochote cha kulipia ada ya viza," alisema Mahamadou Sana, Waziri wa usalama.
Kulingana na huduma ya habari ya serikali, kufuta ada ya viza kwa raia wa bara hilo kunaonyesha kushikamana kwa Burkina Faso na maadili ya Kiafrika (Pan-Africanist), na kukuza ushirikiano wa kikanda.
"Mfumo huu wa viza bila malipo kwa raia wa Kiafrika pia utasaidia kukuza utalii na utamaduni wa Burkinafaso, na kuboresha taswira ya Burkina Faso nje ya nchi," taarifa kutoka huduma ya serikali iliongeza.
Ingawa Waafrika hawatakiwi tena kulipa ada ili kuingia katika taifa hilo la Afrika Magharibi, bado wanalazimika kutuma maombi ya mtandaoni kabla ya kusafiri. Ombi lao litapitiwa na kuidhinishwa, Waziri wa usalama alifafanua.
Burkina Faso, taifa la Sahel ambalo kwa sasa linakabiliwa na vitisho vya usalama kutoka kwa waasi, linaongozwa na mwanajeshi mchanga ambaye amesifiwa kwa msimamo wake wa uafrika.
Kapteni Traoré alichukua madaraka katika mapinduzi ya 2022 lakini tangu wakati huo ameshindwa kutimiza ahadi yake ya kurejesha usalama.
Burkina Faso sasa ni miongoni mwa nchi kama vile Ghana, Rwanda, na Kenya, ambazo hivi majuzi zilipunguza mahitaji ya kusafiri kwa wageni wa Kiafrika.
Bado haijulikani ikiwa hatua hii itasaidia kuboresha taswira ya nchi huku kukiwa na ukosoaji unaoongezeka dhidi ya jeshi.
0 Comments