Wakulima mkoani Mbeya na maeneo ya Nyanda za Juu Kusini wametakiwa kuzingatia ulinzi wa mazingira licha ya shughuli zao za kilimo, ili kusaidia kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.
Kauli hiyo imetolewa na Afisa Mazingira kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Bakari Mwaruma, wakati wa maonesho ya kilimo ya Nane Nane yanayoendelea mkoani Mbeya.
"Baadhi ya shughuli za kilimo kama vile kulima kwenye vyanzo vya maji na kukata miti hovyo, zimekuwa chanzo kikuu cha uharibifu wa mazingira, hali inayochochea mabadiliko ya tabianchi.”
Kwa upande wake, Afisa Mazingira Mwandamizi wa NEMC Mbeya, Tilisa Mwambungu, amesema jitihada mbalimbali zimekuwa zikiendelea kufanyika kwa kushirikiana na wadau ili kuwafikia wananchi na kuwajengea uelewa kuhusu utunzaji wa mazingira.
"Tunatumia redio, mikutano ya kijiji na maonyesho kama haya ya Nane Nane kuwaelimisha wananchi umuhimu wa kulinda mazingira na athari za kutofanya hivyo."
Aidha, NEMC imewataka viongozi wa vijiji na kata kushirikiana kikamilifu katika kutoa taarifa za uharibifu wa mazingira, ili hatua stahiki zichukuliwe kwa wakati.
0 Comments