Header Ads Widget

MACHALI APONGEZA UBUNIFU WA VIJANA WA UDSM NDAKI YA KILIMO, TEKNOLOJIA MAONESHO YA NANENANE DODOMA

 


MWENYEKITI wa Kamati ya Itifaki ya Maonesho ya Wakulima na Wafugaji (Nanenane) Kitaifa mwaka 2025, ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, Moses Machali, amewataka wafugaji wa samaki nchini kujitokeza kwa wingi kutembelea mabanda ya taasisi za elimu ili kujifunza teknolojia mpya zinazoboresha sekta hiyo.

Akizungumza baada ya kutembelea mabanda mbalimbali kwenye maonesho hayo yanayoendelea katika viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma, Machali alisema amevutiwa na ubunifu wa mabinti wanaojihusisha na utengenezaji wa mafuta asilia yanayosaidia kuondoa mikunjo ya ngozi.


Machali pia alieleza kufurahishwa na teknolojia mpya inayotumika katika ufugaji wa samaki, ikiwemo mashine maalum zinazotumika kukamata vifaranga vya samaki bila kutumia mikono, hatua ambayo husaidia kupunguza vifo vya samaki wachanga ambavyo kwa kawaida hujitokeza endapo wanashikwa kwa mikono.

Amesisitiza kuwa matumizi ya teknolojia hizo ni muhimu kwa wafugaji wote wa samaki ili kuboresha uzalishaji na kuokoa mifugo midogo isiyokomaa.

Katika hatua nyingine, Machali amelitaja Banda la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kupitia Ndaki ya Masuala ya Kilimo na Teknolojia, kuwa ni eneo muhimu kwa wakulima na wafugaji kutembelea na kujifunza teknolojia mbalimbali zinazohusiana na kilimo cha kisasa.


Ameeleza kuwa moja ya teknolojia za kuvutia zinazopatikana katika banda hilo ni mtandao wa kidijitali unaowaunganisha wakulima moja kwa moja na maafisa ugani, kwa njia inayofanana na mfumo wa kuomba usafiri kwa kutumia simu za mkononi.


Maonesho ya Nanenane mwaka 2025 yameendelea kuvutia washiriki kutoka sekta mbalimbali, yakiongozwa na kaulimbiu isemayo: “Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.”


MWISHO

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI