Na Hamida Ramadhan, Dodoma
MAMLAKA ya Kusimamia Uvuvi wa Bahari Kuu (DSFA) imefanikiwa kudhibiti uvuvi haramu katika Bahari kuu Tanzania, hatua iliyowezesha ongezeko la mapato mara 10 na kuvutia wawekezaji zaidi katika sekta ya uvuvi wa bahari kuu.
Akizungumza katika Maonesho ya Kilimo ya Nanenane yanayoendelea kwenye viwanja vya Nzuguni, jijini Dodoma, Mkurugenzi Mkuu wa DSFA Dkt. Emmanuel Sweke amesema kuwa mamlaka hiyo imeimarisha usimamizi wa meli za uvuvi kwa kutumia mifumo ya kiteknolojia ya ufuatiliaji wa meli (tega), ambayo inasaidia kufuatilia kwa karibu shughuli za uvuvi kwenye eneo lenye zaidi ya kilomita 2,000 za bahari kuu.
“Kwa sasa hakuna uvuvi haramu katika bahari kuu. Mifumo yetu ya ufuatiliaji imerahisisha usimamizi wa meli zote zilizopata leseni kutoka Tanzania. Meli yoyote inapotia nanga kwenye maji ya Tanzania, inatakiwa kutoa taarifa ndani ya masaa 24,” alisema Dkt. Sweke.
Dkt. Sweke alibainisha kuwa DSFA ndiyo taasisi pekee yenye mamlaka ya kusimamia uvuvi wa bahari kuu, ikiwa na makao makuu yake Zanzibar. Taasisi hiyo pia huandaa na kushauri serikali kuhusu masuala ya sera yanayohusu uvuvi katika eneo hilo.
Aidha, alieleza kuwa taasisi hiyo inasimamia meli zote zinazotumia bendera ya Tanzania zinazovua samaki katika maji ya kimataifa. Samaki wanaosimamiwa wengi wao ni wa aina ya wanaohama kwa haraka (highly migratory species) kama jodari, na kwa sababu hiyo DSFA hushirikiana na nchi nyingine jirani kuhakikisha uhifadhi endelevu.
Akitoa mfano wa mafanikio ya usimamizi, Dkt. Sweke alisema tangu mwaka 2018 DSFA iliwahi kukamata meli moja iliyopatikana na samaki aina ya papa, ambaye ni miongoni mwa spishi zilizopo hatarini kutoweka.
0 Comments