Na Matukio Daima Media
Mkurugenzi Mkuu wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), Dkt. Rose Reuben, ametaja mikakati mbalimbali inayotekelezwa na chama hicho katika kuwalinda na kuwawezesha waandishi wa habari wanawake wanaokutana na changamoto za ukatili wa kijinsia na vitisho sehemu za kazi.
Akizungumza katika mdahalo wa Kitaifa kuhusu Usalama na Ulinzi wa Waandishi wa Habari ulioandaliwa na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) kwa kushirikiana na Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Dkt. Reuben alisema vitisho vya kijinsia vimeendelea kuwa kikwazo kikubwa katika sekta ya habari na jamii kwa ujumla.
Alieleza kuwa aina ya vitisho hivyo ni pamoja na unyanyasaji wa kidijitali kama cyberbullying, trolling na doxxing, unyanyasaji sehemu za kazi, ukatili wa kifamilia na kimapenzi, unyonyaji wa kingono, pamoja na vitisho vya kisiasa.
“Vitendo hivi vinasababisha hofu, vinadumaza ustawi wa wanahabari na kuwanyima fursa za maendeleo,” alisema Dkt. Reuben.
Aliongeza kuwa athari zake ni kubwa kwa waandishi wa habari, hususan wanawake, zikiwemo kusababisha msongo wa mawazo na hofu, kupunguza ushiriki wao katika nafasi za uongozi, kunyamazisha sauti zao katika vyombo vya habari na siasa, kupoteza ajira na fursa za maendeleo, sambamba na kukiuka haki za binadamu.
Akifafanua hatua zinazochukuliwa na TAMWA, Dkt. Reuben alisema chama hicho kimeweka mikakati ya ulinzi ikiwemo kuimarisha sera na utekelezaji wake, kuanzisha madawati ya jinsia katika vyombo vya habari, kutoa msaada wa kisheria, na kuendesha kampeni za uhamasishaji.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ulinzi sehemu za kazi kwa kuboresha sheria zilizopo dhidi ya unyanyasaji kwa kutoa tafsiri iliyo wazi na kuweka mifumo madhubuti ya utekelezaji.
Pia alieleza haja ya kuongeza uelewa na kutoa mafunzo maalum kuhusu ukatili wa kijinsia katika mazingira ya kisiasa, utekelezaji wa sheria, na ufuatiliaji wa uchaguzi, sambamba na kujenga mitandao ya wanawake yenye uwezo wa kusimamia mabadiliko chanya.









0 Comments