Rufiji-Pwani
HATUA ya Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kugawa mitungi ya gesi imepongezwa na wananchii wa Tarafa ya Ikwiriri, Wilayani Rufiji mkoani Pwani, waliopata fursa hiyo, huku wakiomba kuwekewa mfumo unaoweza kusaidia familia zenye kipato cha chini katika ujazaji wa gesi kwa utaratibu wa malipo rafiki.
Katika zoezi la utoaji wa elimu lililoambatana na usambazaji wa mitungi ya Gesi.
Afisa Maendeleo kutoka REA, Bi Raina Diwani Msuya, akitoa elimu kwa wananchi hao amewataka kutumia fursa hiyo vizuri kubadili maisha yao na kulinda afya zao pamoja na mazingira.
Akasema Wilaya ya Rufiji pekee imepokea jumla ya mitungi 3,255 kutoka REA kwa ajili ya kaya mbalimbali ambapo Tarafa ya Ikwiriri imepatiwa mitungi 600 itakayogawiwa katika kata tano za eneo hilo ambazo ni Umwe, Mgomba, Mupi, Ikwiriri na Bwawani Mjini.
Katika ziara hiyo maalum ya utoaji elimu kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia iliyoendeshwa Bi Msuya, wananchi walipata nafasi ya kuelewa faida za matumizi ya Nishati ya Gesi kupikia na namna serikali ilivyodhamiria kulinda afya za wananchi pamoja na mazingira.
Bi Raina Msuya akasema Serikali kupitia REA imeendelea kuhakikisha kuwa nishati safi ya kupikia inamfikia kila mwananchi, hasa waishio vijijini.
"Tumeanza na ruzuku ya mitungi lakini elimu juu ya matumizi yake ni jambo la msingi, vinginevyo hasa kwa afya ya wapishi na ulinzi wa afya na mazingira yetu” alisema
Baadhi ya wananchi wa Ikwiriri akiwemo Aziza Masoud mkazi wa Umwe Kati na Ashura Umwe mfanyabiashara wa chakula walisema hatua ya Serikali kutoa mitungi ya gesi kwa bei ya ruzuku imewasaidia kwa kiasi kikubwa, lakini bado gharama za ujazaji wa gesi ni changamoto.
Wakaishauri Serikali na wadau wengine wa mazingira kushusha bei hiyo kama ilivyofanyika kwenye manunuzi ya mitungi kwani ikiisha ghafla hushindwa kuijaza kwa haraka.
" Kama Serikali ingeweka mfumo wa kulipia kwa pesa ndogo ndogo ingetusaidia sana sisi wanyonge tusio na kipato kikubwa,” alisema Bi Masuod, mkazi wa Umwe Kati
Naye Bi Ashura Juma, muuzaji wa vyakula maarufu kama mama lishe alisema matumizi ya gesi yamerahisisha shughuli zao za kila siku.
“Kupika kwa gesi kunapunguza muda, moshi hakuna, tunafanya kazi katika mazingira mazuri. Ni tofauti kabisa na kutumia kuni au mkaa,” alisisitiza.
Nao Baadhi ya wafanyabiashara wa mkaa akiwemo Ramadhani Mtambo walisema hali imekuwa tofauti kibiashara ambapo biashara yake ya mkaa imeporomoka kutokana na ongezeko la watumiaji wa gesi.
“Soko la mkaa linazidi kushuka,nahitaji msaada ili niweze kufanya biashara ya Gesi lakini naona gharama za kuanza biashara hiyo kwangu Sina,naomba kuwezeshwa kama wafanyabiashara wadogo wa nishati safi na nitaisimamia vyema biashara hii"Alisema Mtambo.
REA kwa sasa inaendelea na kampeni ya kitaifa ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kupunguza athari za kiafya na kimazingira zitokanazo na matumizi ya kuni na mkaa.
0 Comments