Header Ads Widget

MSD YAVUNJA REKODI YA MAKUSANYO SHILINGI BILIONI 397.6 KUKUSANYWA KWA MIAKA MINE

Na Hamida Ramadhan, MatukioDaima Media Dodoma

BOHARI ya Dawa (MSD) imeweka rekodi mpya ya makusanyo ya fedha, baada ya kukusanya jumla ya shilingi bilioni 397.6 kati ya Julai 2021 hadi Juni 2025, ikiwa ni matokeo ya maboresho ya kimfumo na uwekezaji mkubwa wa Serikali katika sekta ya afya.

Katika mwaka wa fedha 2024/2025 pekee, MSD imekusanya shilingi bilioni 184.2, kiwango kikubwa zaidi kuwahi kufikiwa katika historia ya taasisi hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma leo Agosti 15 ,2025 Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amesema kuwa mafanikio hayo ni kielelezo cha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha sekta ya afya inatoa huduma bora na endelevu kwa wananchi wote.

 "Rekodi hii ya makusanyo inadhihirisha kwamba maboresho yanayofanyika kwenye sekta ya afya si ya karatasi tu, bali ni ya vitendo MSD imeimarika, bidhaa za afya zinapatikana, na vituo vya afya vinaendelea kutoa huduma bila kukwama haya ni matokeo ya kazi kubwa inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita,” amesema Msigwa.

Sambamba na makusanyo hayo, MSD imeongeza mapato yake kutoka shilingi bilioni 315.1 mwaka wa fedha 2021/2022 hadi shilingi bilioni 640 mwaka 2024/2025  ikiwa ni ongezeko la shilingi bilioni 325 sawa na asilimia 103.1.

Amesema Kuongezeka kwa mapato hayo kunatokana na uboreshaji wa upatikanaji wa dawa na vifaa tiba, ongezeko la mauzo kwa vituo vya afya, pamoja na ufanisi wa ndani wa taasisi hiyo katika usimamizi wa rasilimali na miundombinu ya usambazaji.

Akdha amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya imetoa jumla ya shilingi bilioni 642.1 kwa MSD kwa ajili ya ununuzi wa bidhaa za afya kwa kipindi cha miaka minne. Kwa mwaka 2024/2025 peke yake, shilingi bilioni 196.3 zimetolewa kati ya bajeti ya shilingi bilioni 200, sawa na asilimia 98 ya fedha zote zilizopangwa kwa vituo vya kutolea huduma za afya.


Msigwa amesema hatua hiyo ni ishara ya uthabiti wa kisera na kisera wa Serikali ya Awamu ya Sita katika kuhakikisha MSD inatekeleza wajibu wake kwa tija.

"Ni mara ya kwanza katika historia ya MSD kuona kiwango hiki cha fedha kikitolewa kwa wakati mmoja. Serikali inatekeleza wajibu wake kwa vitendo, na matokeo yake yanaonekana katika kila mkoa, wilaya na kijiji,” ameongeza Msigwa.

Kwa mujibu wa Msigwa, katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita, zaidi ya shilingi trilioni 8.9 zimetumika katika sekta ya afya, ikiwa ni uwekezaji mkubwa zaidi kuwahi kufanyika.

Uwekezaji huo umewezesha maboresho katika miundombinu ya hospitali, ongezeko la watumishi wa afya, huduma za uchunguzi wa magonjwa, huduma za mama na mtoto, pamoja na upatikanaji wa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi katika hospitali za mikoa na halmashauri.

 “Afya ya Mtanzania ni kipaumbele cha Serikali. Ndiyo maana uwekezaji huu mkubwa unaendelea kufanyika kwa kasi na ufanisi mkubwa lengo letu ni kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora bila kujali anapotoka,” amesema Msigwa.


 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI