Takriban watu 30 wamefariki dunia na zaidi ya 1000 kujeruhiwa katika ajali za barabarani zilizohusishwa na sherehe kubwa ya Magal ya 131 ya Touba, moja ya hafla muhimu zaidi ya kidini nchini humo.
Kulingana na Kamanda Yatma Dièye, mkuu wa Idara ya Habari na masuala ya umma wa Brigade ya zimamoto wa Kitaifa, jumla ya ajali 270 za trafiki zilirekodiwa tangu Jumatatu, Agosti 12, magari mengi yakihusishwa na kusafiri kwenda au kutoka Touba.
Mnamo 2024, karibu watu 700 walikufa katika ajali za barabarani huko Senegal, na 90% ya ajali mbaya zilitokana na makosa ya kibinadamu.
Siku ya Ijumaa, Agosti 15, viongozi wa Senegal walitoa wito wa haraka wa kufuata sheria za trafiki. "Hali hii inahitaji kufuatwa kikamilifu kwa kanuni za trafiki," Kamanda Dièye alisisitiza, akisema kuna hitaji la haraka la uhamasishaji wa pamoja na uwajibikaji barabarani huku serikali ya Senegal ikisisitiza lengo lake la kupunguza ajali za barabarani kwa 50% ifikapo mwaka 2030.
Zaidi ya watu milioni sita walikusanyika Touba - karibu km 150 kaskazini mwa mji mkuu, Dakar - mapema wiki hii.
Hafla kubwa ya Magal ya Touba inaadhimishwa kila mwaka na ‘Mouride brotherhood’, madhehebu la Kiisilamu la Sufi, kwa heshima ya mafundisho na urithi wa mwanzilishi wake, Shaykh Ahmadou Bamba.
Hafla hiyo inaadhimisha kukamatwa kwake na kufukuzwa kwake na viongozi wa kikoloni wa Ufaransa kwenda Gabon mnamo Agosti 12, 1895.
0 Comments