Moto mkali wa nyika kaskazini-magharibi mwa Los Angeles ulisababisha amri ya kuhama kwa maelfu ya wakazi siku ya Ijumaa, kwani joto kali na hali ya ukavu vilichochea kuenea kwake haraka.
Moto huo uliopewa jina la Canyon Fire, uliwaka Alhamisi alasiri kwenye mpaka wa kaunti za Ventura na Los Angeles.
Kufikia Ijumaa jioni, ulikuwa imesambaa kutoka ekari 30 hadi karibu 5,400. Moto huo umedhibitiwa kiasi, huku 28% ya eneo lake ikiwa chini ya udhibiti jioni ya Ijumaa, maafisa walisema, na maagizo ya uokoaji yalipunguzwa hadi kutolewa onyo.
Siku ya Ijumaa usiku, afisa wa zima moto alipata majeraha makubwa wakati lori lao lilipobingirika kwenye kingo na kushuka kwenye mlima, CBS, mshirika wa BBC wa vyombo vya habari vya Marekani, iliripoti.
Wakati joto kali na hali kavu zimekuwa zikitatiza juhudi za kuzima moto, Ijumaa usiku, kaunti ya Ventura ilisema katika taarifa kwamba "hali nzuri ya hali ya hewa" imewaruhusu zima moto kufanya "maendeleo mazuri katika kuzima moto."
Bado kulikuwa na maafisa zima moto 400 waliokuwa wakipambana na moto huo Ijumaa jioni. Moto bado unaendelea na unasambaa mashariki kuelekea Castaic katika Kaunti ya Los Angeles, mamlaka ilisema.
Huku utabiri wa halijoto ukiongezeka hadi 100°F (37.7°C) katika siku zijazo, wakazi wanahimizwa kukaa macho. Katika jiji la Santa Clarita, mojawapo ya maeneo yaliyo karibu na moto huo, wakazi wametakiwa kukaa mbali na maeneo yaliyoathiriwa na moto.
0 Comments