Na Hamida Ramadhan,Matukio DaimaMedia Dodoma
MGOMBEA Urais kupitia Chama cha Sauti ya Umma (SAU), Majalio Paul Kyara, leo Agosti 13 amechukua fomu ya kuwania nafasi ya Urais katika ofisi za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) akiwa mgombea wa 13 kufanya hivyo.
Akizungumza baada ya kuchukua fomu , Kyara akiwa ameambatana na mgombea mweza Satia Mussa Bebwa amesema serikali yake, endapo itapata ridhaa ya wananchi, inalenga kutengeneza ajira milioni 10 ndani ya kipindi cha miaka mitano.
Amesema serikali ya SAU italeta mapinduzi ya kiuchumi kupitia sekta ya viwanda, kilimo na teknolojia, ikiwa ni hatua ya kumkomboa Mtanzania kutoka kwenye umasikini ambapo mwelekeo huo utasaidia kupunguza gharama za maisha na kuongeza fursa za ajira kwa vijana.
Kwa upande wa nishati, Kyara amesema serikali yake itashughulikia changamoto ya gharama ya umeme kwa waendeshaji wa biashara ndogo na viwanda, sambamba na kushirikiana na kampuni mbalimbali ili kuimarisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa Watanzania wa kawaida.
Katika sekta ya elimu, mgombea huyo ameahidi kurejesha maslahi ya walimu, kuboresha mazingira ya kufundishia, miundombinu ya shule pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa vitabu vya kufundishia kwa urahisi kwani elimu bora ni msingi wa taifa imara na lenye maendeleo.
Aidha, serikali ya SAU imepanga kuzindua rasmi ilani ya uchaguzi ndani ya siku 40, ikiwa pamoja na kurudisha mchakato wa kupata Katiba mpya. Kyara amesema lengo la chama chake ni kujenga serikali na taifa lenye uadilifu kwa kuongozwa na watu wenye hofu ya Mungu.
Ameongeza kuwa SAU itapambana na tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana, kupunguza bei za mafuta kwa wananchi wa maeneo ya pembezoni na kuhakikisha maendeleo yanawafikia Watanzania wote bila ubaguzi.
0 Comments