Header Ads Widget

MGOMBEA URAIS ADA-TADEA AGEUKIA MAPINDUZI YA AI, ATOA WITO WA MAGEUZI YA FIKRA NA TEKNOLOJIA


Na  Hamida Ramadhan, MatukioDaima Media Dodoma

 MGOMBEA wa urais kupitia Chama cha African Democratic Alliance Party (ADA-TADEA),  Georges Gabriel Bussungu, amechukua fomu ya kuwania nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania huku akiweka wazi dhamira yake ya kuleta "mapinduzi ya njano" yanayolenga katika fikra, teknolojia, na uchumi wa kisasa unaotegemea akili mnemba (AI).

Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa fomu na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Mhe. Jaji Jacobs Mwambegele, Bussungu alisema Tanzania haiwezi kuendelea kubaki nyuma katika dunia ya leo ambayo inaendeshwa na teknolojia ya akili bandia.


 "Ulimwengu umebadilika. Sasa ni zama za akili mnemba Artificial Intelligence. Tunahitaji si tu viongozi, bali taifa lenye fikra mnemba, ambalo linaweza kuongoza mageuzi ya kiteknolojia, kielimu, na kiuchumi kwa faida ya Watanzania wote," amesema Bussungu.

Akiwa ameambatana na mgombea mwenza wake, Mhe. Ali Makame Issa, Bussungu ameeleza kuwa "Mapinduzi ya Njano" ni dira ya ADA-TADEA katika uchaguzi huu, yakilenga kuondoa utegemezi wa kiakili na kiuchumi, na kuandaa taifa lenye uwezo wa kushindana katika soko la dunia linalozidi kutawaliwa na teknolojia bunifu.

 “AI si adui, bali ni fursa. Tukiiogopa, tutabaki nyuma ADA-TADEA inaamini kuwa akili mnemba inaweza kutumika katika kuboresha kilimo, elimu, afya na hata mifumo ya usimamizi wa rasilimali,” alisisitiza.

Katika hatua hiyo, Bussungu pia ametoa salamu za rambirambi kwa familia ya Job Ndugai, Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliyefariki dunia hivi karibuni, akisema msiba huo ni pigo kwa taifa na historia ya Bunge.


Kwa mujibu wa ADA-TADEA, manifesto yao kamili inayochochewa na dira ya AI na mageuzi ya karne ya 21 itazinduliwa rasmi mara baada ya kukamilika kwa mchakato wa uteuzi wa wagombea.

Mpaka sasa, wagombea saba tayari wamechukua fomu za urais, akiwemo Rais wa sasa Samia Suluhu Hassan (CCM) Coaster Kibonde (Chama Makini),Doyo Hassan Doyo (NLD),Kunje Ngombare Mwiru (AAFP) Hassan Almas (NRA) na Twalib Kadege (UPDP).

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI